DKT. BITEKO ATAKA TATHIMINI IFANYIKE KWA HAKI KULETA MATOKEO



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wataalam wa ufuatiliaji na tathmini nchini kufanya kazi yao kwa kizingatia misingi ya kitaaluma ili kuleta matokeo.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 12, 2025 wakati akimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah kufunga Kongamano la nne la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) lililofanyika Jijini Mwanza.

“ Mnapofanya kazi zenu msijione wanyonge wala msitafute kupendwa bali tendeni haki kwa kutuonesha udhaifu uliopo na kuonesha ukweli ili - ufanyiwe kazi” amesema Dkt. Biteko.


Amewahimiza wataalam hao kufanya kazi bila kuhurumiana na badala yake kuwa wakweli kwa kuonesha mafanikio nanudhaifu uliopo ili kuleta ufanisi.

Katika hatua nyingine, amewapongeza wataalam wa ufuatiliaji na tathmini kwa kutekeleza maazimio ya mwaka uliopita kwa asilimia 78 na kuongeza kwa kuwataka kuongeza nguvu zaidi katika sekta hiyo.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya thathmini ya maazimio yaliyofikiwa mwaka jana, lakini tunahitaji zaidi kutoka kwenu.” amesisitiza.

Aidha, Dkt. Doto Biteko amewaelekeza waajiri, wakurugenzi na wakuu wa idara na vitengo kuwapeleka wataalam wao katika mafunzo zaidi ya kitaalam ili waweze kupata mbinu na ujuzi wa kufanya majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Dkt. James Kilabuka amesema Kongamano la mwaka huu limewavutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Mwaka huu tumepata washiriki zaidi ya 1,200 ikilinganishwa na washiriki 954 wa mwaka jana” amesema Dkt. Kilabuka

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuimarisha uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa Jamii ili kuwezesha utendaji bora na Maendeleo endelevu”.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO