OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAWATAKA WAHARIRI KUENDELEA KUZINGATIA MAADILI NA KATIKA KUCHANGIA AMANI YA TAIFA*
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewataka Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuzingatia maadili na kutumia kalamu zao kwa uadilifu katika kuhabarisha umma, kwa kuangazia umuhimu wa kulinda amani na usalama wa taifa wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Ipyana Mlilo, wakati wa kufunga kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Septemba 12, 2025 jijini Dodoma.
Bw. Mlilo amesema kuwa Sekta ya Habari ni muhimu katika taifa, hivyo kupitia kikao hicho kimetoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri, ili kufanikisha utoaji wa elimu kwa jamii kwa weledi .
“Kikao kazi hiki kimekuwa na manufaa makubwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa mpana kuhusu masuala ya kisheria. Tumejadiliana mambo mengi na yote yamepokelewa kwa uzito; tutayafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuelimisha umma." Amesema Bw. Mlilo.
Akielezea majukumu ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) katika kikao kazi hicho Rais wa Chama hicho, Bw. Bavoo Junus, amesema kuwa TPBA ni nguzo muhimu katika kulinda, kusimamia na kutetea maslahi ya taifa na rasilimali zake.
Ameeleza kuwa TPBA ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wote wanaohudumu katika ofisi za umma kama ikiwemo halmashauri, wizara, wakala, taasisi za serikali, na Kampuni ambazo Serikali ina hisa.
“Tuna jukumu la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya sheria. Hili limefanikiwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambayo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Bw. Junus.
Amefafanua kuwa TPBA, kupitia umoja wake, imeunda jukwaa la kuwaunganisha Mawakili wa serikali ambapo wamekuwa wakijadiliana kuhusu taaluma zao, pamoja na kutetea maslahi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, amesema kuwa Chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo endelevu kwa wanachama wake ili kukuza ufanisi na uelewa wa mfumo wa Sheria nchini, badala ya kusubiri waajiri kutekeleza jukumu hilo.
“Tumeendelea kutoa elimu ya Sheria kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kuandaa makongamano ya kisheria yanayolenga kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya kisheria,” amesema Junus.
Amesema kuwa TPBA kilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 16A(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268, pamoja na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti 2019.
Aidha, Bw. Junus ameeleza kuwa TPBA na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ni vyama viwili tofauti; ambapo TPBA ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wanaohudumu Serikalini pekee, ilhali TLS ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wote nchini bila kujali mwajiri wao.
Akizungumza kwa niaba ya Wahariri walioshiriki kikao kazi hicho, Mhariri Mkuu Clouds Media Bi. Joyce Shebe, ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu kikao kazi hicho ambacho kimekuwa na manufaa makubwa katika kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa mambo mbalimbali ya kisheria jambo ambalo litasaidia kutekeleza majukumu yao Kwa ufanisi.
Comments
Post a Comment