TUME YA MADINI, BOT NA FIU ZAKUTANA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UTAKATISHAJI FEDHA SEKTA YA MADINI*



Dodoma, Septemba 12, 2025

Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imekutana na wataalam kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit – FIU) kwa lengo la kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti utakatishaji fedha katika sekta ya madini.

Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Tume ya Madini jijini Dodoma kimekusudia kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo tatu ili kuzuia mzunguko wa fedha haramu kupitia miamala ya wadau wa sekta ya madini.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Annasia Kwayu, amesema kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika mnyororo mzima wa biashara ya madini. 


Ameongeza kuwa Tume inatambua na kuthamini mchango wa FIU katika kutoa miongozo na mafunzo yanayosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu.

“Tumejadili masuala mbalimbali na wenzetu kutoka BOT na FIU. Jambo kubwa ni kudhibiti utakatishaji fedha katika sekta ya madini ili kulinda heshima ya nchi kimataifa na kuongeza mchango wa sekta hii katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema Kwayu.

Kwa upande wake, Dkt. Anna Lyimo kutoka Benki Kuu (BoT) amesema Benki Kuu, kama ilivyo kwa benki kuu za mataifa mengine, ina jukumu la kusimamia sera ya fedha na kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.

“BoT imejipanga kikamilifu kudhibiti mianya ya utakatishaji wa fedha haramu katika zoezi la ununuzi wa asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa nchini, na tupo tayari kushirikiana na Tume ya Madini ili kuhakikisha nchi inaendelea kuaminika kimataifa na kukuza uchumi wake,” amesema Dkt. Lyimo.


Naye Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), Majaba  Magana, amesisitiza kuwa Tume ya Madini kama taasisi yenye dhamana ya kudhibiti utakatishaji fedha katika sekta ya madini, inatakiwa kuimarisha mifumo yake ikiwemo kuandaa miongozo ya utekelezaji ikiwa ni sehemu ya Mwongozo wa Usimamizi uliotolewa na FIU.

“Kwa upande wetu, tupo tayari kutoa ushirikiano wa karibu, ikiwemo kusaidia katika utoaji wa elimu kwa wadau wa sekta ya madini ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo,” amesema Magana.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO