MHE. SALOME AKUTANA NA KAMPUNI ZA CHINA KUJADILI UWEKEZAJI KATIKA MAFUTA, GESI ASILIA NA NISHATI JADIDIFU*



Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome  Makamba, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni mbili kutoka China kwa lengo la kujadili  uwekezaji katika sekta ya nishati nchini, hususan katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya gesi pamoja na miradi ya nishati jadidifu.

Katika kikao kilichofanyika Oktoba 23, 2026, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati, Dar es Salaam,
Mhe. Salome amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya ChuanQing Drilling Company, Bw. Liu Chang Xu, yaliyolenga kujadili fursa za uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ujenzi wa miundombinu katika mkondo wa chini wa sekta ya petroli pamoja na miradi ya nishati jadidifu, hususan nishati ya jua na jotoardhi.

Pia, Mhe. Salome amezungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kwala Industries, Bw. Janson Huang, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Kinyerezi, Dar es Salaam, hadi Chalinze mkoani Pwani, unaoendelea kusimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Mradi huo unatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya viwanda katika eneo la Chalinze na maeneo jirani, hatua itakayochochea uwekezaji na kukuza shughuli za kiuchumi.

Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Mafuta na Gesi), Dkt. James  Mataragio, pamoja na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).


Comments

Popular posts from this blog

NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi

DC Mnzava akabidhiwa hati ya Pongezi na CCM kwa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani

OFISI ZA MADINI NCHINI ZATAKIWA KUIMARISHA ELIMU YA ULIPAJI KODI*