WIZARA YA NISHATI YAWASILISHA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SEKTA NDOGO YA MAFUTA NA GESI ROBO YA KWANZA 2026/27



Dodoma, Oktoba 22, 2026

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, leo Oktoba 22, 2026, amewasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27, katika sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia.

Kikao hicho kimefanyika katika Kumbi za Bunge jijini Dodoma, chini ya uenyekiti wa Mhe. Subira Mgalu, ambapo Wizara imewasilisha maendeleo ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohusu utafiti, uzalishaji na matumizi ya mafuta na gesi asilia nchini.

Katika maeneo ya vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2026/27, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza hatua za utekelezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (Tanzania Liquefied Natural Gas – TLNG), kuimarisha utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za petroli katika vitalu vya kimkakati vya Lindi- Mtwara, Songo Songo Magharibi, Eyasi- Wembere na Mnazi Bay Kaskazini.

Aidha, TPDC imeeleza utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia, ikiwemo bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba, Dar es Salaam hadi Chalinze, pamoja na bomba la usambazaji wa gesi kutoka Kisemvule hadi Mbagala.

Kwa upande wake, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeeleza hatua za kuendelea kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia nchini, pamoja na maandalizi ya Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa juhudi zinazofanyika katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya sekta ya nishati nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe wa Kamati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Ndg. Mussa Makame; Mkurugenzi Mtendaji wa PURA, Mha. Charles Sangweni; Mkurugenzi  TANOIL, Ndg. James Sanawa, pamoja na wataalamu kutoka Wizara na taasisi zake.




Comments

Popular posts from this blog

NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi

DC Mnzava akabidhiwa hati ya Pongezi na CCM kwa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani

OFISI ZA MADINI NCHINI ZATAKIWA KUIMARISHA ELIMU YA ULIPAJI KODI*