WANANCHI MAFISA WALIA NA UKABAJI MOROGORO

WANANCHI MAFISA WALIA NA UKABAJI MOROGORO.

Mafisa, Morogoro.

Wananchi wa Kata ya Mafisa, Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro, wamewasilisha kero mbalimbali za kiusalama kupitia programu ya Ongea na Kamanda, iliyofanyika Oktoba 17, 2026, wakilalamikia vitendo vya ukabaji na changamoto nyingine zinazowakabili katika maeneo yao.

Akizungumza katika programu hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, ametoa elimu kuhusu kujiepusha na utapeli wa kimtandao na matumizi ya dawa za kulevya, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuchangia kujiingiza katika uhalifu, ikiwemo wizi na ubakaji.
Miongoni mwa kero zilizowasilishwa na wananchi ni vitendo vya ukabaji, ikiwemo madai ya kuwepo kwa kundi linalojulikana kwa jina la Warusi linalodaiwa kujihusisha na uhalifu huo. Changamoto nyingine zilizotajwa ni baadhi ya wazazi kuwatetea watoto wanaojihusisha na uhalifu, lugha isiyofaa inayodaiwa kutumiwa na baadhi ya askari wanapohudumia wananchi, pamoja na watuhumiwa kukamatwa na kuachiwa bila kuchukuliwa hatua.

Akijibu hoja hizo, ACP Kantimbo amewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia mwenendo wao ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya uhalifu. Kuhusu malalamiko ya lugha inayotumiwa na baadhi ya askari, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhudumiwa kwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa kwa wakati wanapokutana na changamoto katika huduma wanazopata. Kuhusu watuhumiwa kukamatwa na kuachiwa, ameeleza kuwa ushahidi ni muhimu katika mwenendo wa mashauri ya jinai mahakamani, akiwahimiza walalamikaji kujitokeza kutoa ushahidi wanapohitajika.
Kufuatia malalamiko ya ukabaji, ACP Kantimbo amemwelekeza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro, SSP Oscar Ngumbulu, kufuatilia taarifa za kundi linalodaiwa kujihusisha na vitendo hivyo katika Kata ya Mafisa ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki. Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na kushiriki kikamilifu katika kudumisha usalama wa jamii.






#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX karibu sana.

Comments

Popular posts from this blog

NMB Same Yachochea Ari ya Mafanikio kwa Wanafunzi, Yasema “Bidii, Nidhamu na Malengo” Ndio Siri ya Ushindi

DC Mnzava akabidhiwa hati ya Pongezi na CCM kwa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani

OFISI ZA MADINI NCHINI ZATAKIWA KUIMARISHA ELIMU YA ULIPAJI KODI*