APP YA MKULIMA YAFUNGUA MILANGO YA MAARIFA KWA WAKULIMA

Tembelea Channel yetu ya Youtube uweze ku Subscribe kwa taarifa zaidi.

APP YA MKULIMA YAFUNGUA MILANGO YA MAARIFA KWA WAKULIMA

Na Christina Thomas,

Morogoro.

Katika dunia inayokua kwa kasi kiteknolojia, upatikanaji wa taarifa sahihi na za kisasa umekuwa nguzo muhimu katika kuongeza tija kwenye kilimo na ufugaji. Dhana hii imesukumwa mbele na Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SUA) kupitia App ya Mkulima, programu inayosogeza machapisho ya kilimo moja kwa moja kwa mkulima kupitia simu za mkononi.

App hii, iliyozinduliwa na Maktaba ya Taifa ya SUA chini ya usimamizi wa wataalamu wa habari na maktaba, inalenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa taarifa za kisayansi na mbinu bora za uzalishaji. Kupitia programu hiyo, wakulima na wananchi sasa wanaweza kusoma machapisho, tafiti, na miongozo mbalimbali bila kulazimika kufika maktabani au kutumia kompyuta.

Jabir Jabir, Mkutubi na Msimamizi wa Kitengo cha Rejea na Machapisho kwa Jamii kutoka Chuo Kikuu cha SUA, amesema kubuniwa kwa App ya Mkulima ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha Mkulima Collection ghala la taarifa za kilimo linalohifadhi machapisho mbalimbali yanayohusu uzalishaji bora na kuongeza mapato.

“Awali, huduma za Mkulima Collection zilipatikana zaidi kwa watumiaji wa kompyuta kupitia tovuti ya SUA. Tuliona haja ya kuwasogezea taarifa wale wanaotumia simu za mkononi, hasa wakulima walioko vijijini. Sasa, kupitia App ya Mkulima, taarifa zinapatikana kwa haraka, urahisi, na bila gharama kubwa,” amesema Jabir.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maktaba, App hiyo tayari inapatikana kwenye Google Play Store na inaweza kupakuliwa bure. Baada ya kupakua, mtumiaji anaweza kuifungua na kuvinjari machapisho mbalimbali ya kilimo, mifugo, na masuala ya mazingira kwa lugha rahisi na nyepesi.

Jabir amesisitiza umuhimu wa wakulima na wananchi kwa ujumla kujenga tabia ya kusoma na kufuatilia taarifa mpya, akibainisha kuwa maarifa hubadilika kwa kasi kutokana na mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya teknolojia.

“Taarifa za zamani zinaweza kutoendana na changamoto za sasa. Kupitia App ya Mkulima, wakulima wanaweza kupata maarifa mapya yanayokwenda na wakati, na hivyo kuongeza uzalishaji na ufanisi,” amesema Jabir.

Katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, huduma ya Mkulima Collection imetolewa kwa njia ya nakala ngumu na kidijitali, jambo lililovutia wakulima, watafiti, wanafunzi, na viongozi wa sekta ya kilimo waliotembelea banda la SUA.

Baadhi ya wakulima na wafugaji waliohudhuria maonesho hayo wamesema kuwa hatua ya SUA kuanzisha App ya Mkulima inawarahisishia kufuatilia maendeleo ya teknolojia mpya za kilimo na ufugaji, na pia inawaunganisha moja kwa moja na vyanzo vya maarifa vya kuaminika. Wamesema kusoma kwenye simu kumewasaidia kutatua changamoto kwa wakati, bila kusubiri mikutano au mafunzo ya ana kwa ana.

Mariam Ally Mussa, mkulima kutoka Wilaya ya Mvomero, amesema App hiyo imewasaidia kupata maarifa ya kupanda mbegu bora za mihogo na mahindi kwa tija kubwa.

“Nilipata changamoto ya kupata taarifa za kisasa za kilimo chenye kuhimili ukame. Sasa naweza kusoma mwongozo kwenye simu hata nikiwa shambani, na kuona hatua zote za uzalishaji,” amesema Mariam.

Kwa mujibu wa SUA, lengo la kuanzisha App ya Mkulima ni kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa taarifa, kuharakisha uenezaji wa teknolojia za kisasa za kilimo, na kuhakikisha wakulima wote, hata walioko mbali na miji, wanapata maarifa yanayolingana na mahitaji yao ya kila siku.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na mifugo, kupunguza gharama za uzalishaji, na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Pia, inapoongeza maarifa kwa wananchi, inachangia kukuza uchumi wa taifa kupitia kilimo chenye tija na biashara ya mazao yenye thamani kubwa.

https://youtu.be/0jrKV4xGqkE?si=5GmZBjTCiRIBFNg8

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO