DC TABORA: AFYA YA MIFUGO NI NGUZO YA UCHUMI WA TAIFA.

DC TABORA: AFYA YA MIFUGO NI NGUZO YA UCHUMI WA TAIFA. 

Na Musa Mathias,
Tabora.

Katika kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya homa ya mapafu kwa mifugo, Serikali wilayani Tabora imezindua rasmi zoezi la uchanjaji wa mifugo, tukio lililofanyika katika Kata ya Iteemia wilayani Tabora.

Zoezi hili linatajwa kuwa suluhisho la muda mrefu katika kulinda afya ya mifugo na kuongeza thamani yake katika soko la ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo Wella, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametoa fedha nyingi kuhakikisha chanjo hizi zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wafugaji wote nchini.

Pia amewapongeza wafugaji kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo, akibainisha kuwa ushirikiano wao ni kielelezo cha uelewa wa thamani ya mifugo katika kuinua kipato cha kaya na kukuza uchumi wa Taifa.

Vilevile, amewashukuru wataalam wa mifugo kwa kujitoa kwa moyo mmoja kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi na weledi mkubwa.

Aidha, Bi. Wella amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu afya ya mifugo, kwani kufanya hivyo ni sawa na kulinda ajira, kipato na chakula cha maelfu ya wananchi. Amewataka wafugaji kuendelea kushirikiana na wataalam wa mifugo katika kuhakikisha kila mnyama anapatiwa chanjo na matibabu stahiki.

Kwa ujumbe wake wa mwisho, ameeleza kuwa: “Tukilinda mifugo yetu, tunalinda uchumi wetu, tunatengeneza familia imara na kuandaa kizazi chenye maisha bora na salama.”





Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO