WAZIRI JAFO: TANZANIA YANUFAIKA NA BIASHARA ZA NDANI NA NJE, MAUZO YAONGEZEKA.


Na,Agnes Mambo,Tanga.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema Tanzania inaendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa kupitia biashara za ndani na nje, huku uwiano wa biashara ukiimarika kwa kasi katika masoko ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumza jijini Tanga Agosti 20/2025  wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Maofisa Biashara nchini (MAW), Dkt. Jafo amesema uwiano wa biashara katika kanda ya Afrika Mashariki umeongezeka kutoka dola za Kimarekani bilioni 1.62 hadi bilioni 1.63. Aidha, kwa nchi wanachama wa SADC, mauzo yameongezeka kutoka dola bilioni 1.2 hadi kufikia bilioni 2.9, sawa na ongezeko la asilimia 127.

“Haya ni mafanikio makubwa, na ninyi maofisa biashara mna mchango mkubwa katika hili. Katika maeneo yenu ya serikali za mitaa, ambapo mazao yanauzwa na biashara zinafanyika, ninyi ndio mnasimamia shughuli hizi. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri,” amesema Dkt. Jafo.


Ameongeza kuwa hata kwenye soko la Ulaya, mauzo ya Tanzania yameongezeka kutoka dola milioni 840 hadi kufikia wastani wa dola bilioni 2.3, jambo linaloonesha kuwa jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zinaendelea kuzaa matunda.

“Leo hii tuna kila sababu ya kujivunia. Rais wetu amewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye mifumo ya biashara, lengo likiwa ni kutengeneza mazingira bora ya ndani na kuvutia wawekezaji. Matokeo yake ni mafanikio makubwa ya kiuchumi,” amefafanua.

Dkt. Jafo amesema kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, idadi ya viwanda nchini imeongezeka kutoka 52,800 hadi kufikia takribani 80,000, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya viwanda 18,000. Kati ya hivyo, viwanda vingi ni vidogo, ambavyo vina mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa ndani na kusaidia mchakato wa uwekezaji na biashara.


Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiukabili mkoa huo ilikuwa ni kufa kwa viwanda. Hata hivyo, amesema baadhi ya viwanda hivyo tayari vimeanza kufufuliwa huku vingine vikiwa katika hatua za mwisho za kufunguliwa.

"Baadhi ya viwanda vilivyofufuliwa ni pamoja na kiwanda cha kusindika samaki, kiwanda cha sabuni, na pia tunaelekea kufungua kiwanda cha kutengeneza magari ya wagonjwa. Tutaendelea kuhakikisha viwanda vinazinduliwa na vinafanya kazi kwa tija," amesema Dkt. Burian.

Akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Biashara nchini, Bi. Elizabeth Swagi, ameeleza kuwa uhaba wa vitendea kazi katika ofisi zao umekuwa changamoto kubwa inayokwamisha utoaji wa huduma kwa jamii kwa ufanisi. Ameiomba serikali kushughulikia changamoto hiyo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Sekta ya Mavazi Yachangia Maendeleo ya Uchumi

Sekta ya mavazi (clothing and apparel industry) nchini Tanzania imeendelea kuwa moja ya maeneo muhimu yanayochochea ajira, ubunifu na maendeleo ya viwanda. Kwa sasa, viwanda vya ushonaji, utengenezaji wa nguo, na usindikaji wa malighafi kama pamba vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa ndani. Aidha, vijana wengi wamepata ajira kupitia shughuli za ushonaji, ubunifu wa mitindo (fashion design), na biashara ya mavazi ya mitumba na mapya.

Soko la mavazi lina nafasi kubwa katika biashara ya ndani na nje ya nchi, hasa kupitia usafirishaji wa bidhaa za kitamaduni, vitenge, na vazi la kiafrika ambalo limeendelea kuvutia mataifa mengi barani Afrika na duniani kote. Ili sekta hii izidi kustawi, serikali na wadau binafsi wanahimizwa kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ya ushonaji, mafunzo kwa vijana, na kuboresha miundombinu ya viwanda vidogo na vya kati.



 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO