REA YATEKELEZA KWA VITENDO MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
📌REA KUANZA UUZAJI NA USAMBAZAJI MAJIKO BANIFU 6,488 MKOANI SONGWE
📌MAJIKO BANIFU 1,622 KUSAMBAZWA KILA WILAYA
📍 SONGWE
Wakazi wa mkoa wa Songwe waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira na afya zao kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 28, 2025 wakati wa utambulishaji wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu mkoa wa Songwe na mhandisi wa miradi kutoka wakala wa nishati vijijini, Kelvin Tarimo.
Mhandisi Tarimo amesema, serikali kupitia wakala wa nishati vijijini imeandaa mpango wa utekelezaji mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la zaidi ya asilimia themanini 80% ya watanzania ifikapo 2034 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mhandisi Tarimo ameendelea kwa kusema, katika kutekeleza mradi huu, Wakala wa Nishati Vijijini umeeandaa mpango wa uuzwaji wa majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku yenye ufanisi mkubwa katika utumiaji wake
Kwa mkoa wa Songwe, mradi huu unatarajia kugharimu zaidi ya TZS Milioni 371.1 wakati wa utekelezaji wake na majiko 6,488 kusambazwa katika wilaya nne za mkoa wa Songwe ambazo ni wilaya ya Momba, Mbozi, Ileje na Songwe ambapo kila wilaya itapata majiko 1,622.
Mhandisi Tarimo amesema mikataba ya mradi huu ilisainiwa tarehe 09 Mei, 2025 kati ya REA na mtoa huduma kampuni ya Greenway Grameen Infra Pvt Limited na ECOMAMA Tanzania Limited.
Mtoa huduma atauza na kusambaza majiko kwa bei ya ruzuku. Gharama ya jiko moja ni TZS 71,500 lakini serikali imetoa ruzuku ya asilimia 80 hivyo mwananchi atanunua kwa gharama ya TZS 14,300 tu.
Akipokea taarifa ya mradi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dkt. Frank George Haule Hawasi amesema,
"Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama na ya kupikia na kuwasihi wananchi kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa majiko haya banifu ambayo ni nafuu kwa gaharama na ufanisi mkubwa katika utumiaji wake.
Naye mwakilishi wa kampunj ya Greenway Gramen Infra Pvt Limited na ECOMAMA Tanzania Limited, ndugu Godfrey Komanya amesema,
" Mradi wetu huu unakuja kubadilisha mtazamo wa wananchi katika matumizi ya nishati ya kupikia kutoka kutumia Nishati zisizo salama za kupikia na kuanza kutumia nishati safi na salama za kupikia"
Comments
Post a Comment