DC SHAKA: VIJANA MUWE NGUZO YA USALAMA NA MAENDELEO YA TAIFA

DC SHAKA: VIJANA MUWE NGUZO YA USALAMA NA MAENDELEO YA TAIFA

Na Christina Thomas, 

Kilosa, Morogoro.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka vijana kote nchini kuendelea kuwa safu ya mbele katika kulinda usalama na mshikamano wa Taifa, akisisitiza kuwa hakuna maendeleo bila mazingira salama.

Akizungumza leo wakati wa kufunga mafunzo ya miezi minne kwa askari 114 wa Jeshi la Akiba (Mkupuo wa 20), yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mvumi, DC Shaka alisema usalama ni msingi wa ustawi wa uchumi, hasa kwa maeneo yenye rasilimali muhimu kama Morogoro na Kilosa.

“Jeshi la Akiba ni nguzo muhimu katika mfumo wa ulinzi wa Taifa letu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua wajibu wa kila raia kulinda uhuru, umoja, na usalama wa nchi yetu,” alisema.

Alitoa pongezi kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Makao Makuu na Kamandi ya Jeshi la Akiba kwa uratibu wa mafunzo yenye weledi na uzalendo, hatua inayoongeza idadi ya askari kila mwaka wilayani Kilosa.

Kwa kuwatia moyo wahitimu, DC Shaka aliwataka kuhakikisha mafunzo waliyopata yanatafsirika katika vitendo vya kila siku kwa kudumisha nidhamu, utiifu, na kujitolea katika huduma kwa Taifa.

“Mkiwa uraiani, ndeleeni kuwa mfano wa nidhamu, utiifu na uzalendo. Mnapoitwa kwa majukumu ya Taifa, jitokezeni bila kusita, mkiweka mbele maslahi ya nchi kuliko ya binafsi,” aliongeza.

Aidha, aliwaasa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kudhibiti majanga, kulinda raia, na kuzuia vitendo vya uhalifu kupitia utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati.

DC Shaka alihitimisha kwa kuwataka vijana hao kuwa mabalozi wa amani na mshikamano, akibainisha kuwa Jeshi la Akiba ni chelezo la Taifa linalochangia kulinda dira ya maendeleo inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.





Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO