WAGOMBEA,WANACHAMA WA CCM VILIO JUU YA KURA ZA MAONI HAI
Na Mwandishi wetu,Kilimanjaro.
Hai. Mchakato wa kura za maoni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Hai, Kilimanjaro, umelalamikiwa na baadhi ya wagombea na wanachama wakidai umejaa dosari ikiwemo rushwa, usafirishaji wa wajumbe na upendeleo wa wazi kutoka kwa baadhi ya viongozi.
Wanachama hao wamedai kuwa licha ya chama kuwa na utaratibu wa kuhakikisha uchaguzi wa ndani unasimamiwa kwa haki, wilayani Hai kulikuwa na changamoto nyingi zenye kuondoa uhalali wa mchakato huo.
Baadhi ya hoja zilizotolewa ni pamoja na majina ya wajumbe halisi kutokuwa bayana, kuruhusiwa kwa wajumbe wasio halali, huku wengine wakidaiwa kupiga kura zaidi ya mara moja.
Aidha, makatibu wa kata walitajwa kushiriki kampeni za kumpigia debe aliyekuwa Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe.
Katika Kata ya Machame Kaskazini, Katibu wa Kata, Silaa, alisimamishwa baada ya kudaiwa kuandika barua kwa makanisa na misikiti akihimiza wananchi kumpigia kura Mafuwe.
Inadaiwa kuwa katika kata za Masama, Rundugai na Machame Mashariki, walikamatwa watu wakiwa na karatasi za kura zilizokwisha kupigwa.
Wanachama hao walidai pia kuwa siku ya kura za maoni baadhi ya wajumbe walisafirishwa kwa magari na kugawiwa fedha, wakisema kila mmoja alipokea Sh50,000 na maelekezo ya namna ya kupiga kura.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Hai nao walitajwa kuingilia mchakato, akiwemo Mwenyekiti wa UWT Wilaya, Happiness Kimaro (Mama Mkami), aliyedaiwa kutoa maelekezo ya kumpigia kura Mafuwe katika Kata ya Masama Mashariki.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu tuhuma hizo, Katibu wa CCM Wilaya ya Hai, Hamis Mkaruka Kura, alisema wamesimamisha Katibu Kata wa Machame Kaskazini kwa madai ya kukiuka utaratibu baada ya kuandika barua makanisani na misikitini akihimiza waumini wamchague Saashisha Mafuwe.
"Uchaguzi ulienda vizuri tu; sasa wanapodai kuwa makatibu kata waliharibu kura za maoni kwa kuwa wapiga kampeni sio kweli; wanatokaje katika vyumba vya kupigia kura wakati wao ni wasimamizi, mengine ni hearsay (maneno ya kusikia)", alisema Katibu huyo.
Katibu huyo aliongeza kwa kusema tuhuma za rushwa ni mambo ya kusikia kwani hadi sasa hajaletewa ripoti yoyote ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu vitendo vya rushwa wakati wa kura za maoni wilaya ya Hai zilipofanyika.
Mgombea ubunge wa Jimbo hilo Saashisha Mafuwe ambaye yupo katika kinyanganyiro ndani ya chama katika nafasi hiyo alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo alikataa kuzungumza akisema mambo yote chama ndicho kinasimamia.
"Kwa sasa siwezi kusema lolote; kama unataka kuhusu hayo kawaone chama watakueleza mimi kwa sasa hapana", alisema Mafuwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, alipoulizwa kama kuna watia nia wanaoshikiliwa na hatua zinazochukuliwa hususan wilayani Hai, alisema:
“Leo ni Jumapili, naweza nisiwe na takwimu. Ukihitaji taarifa njoo ofisini ndio utapata.Mimi nitakuwa nje kwa wiki mbili, lakini hata nisipokuwepo ofisi ipo na kuna watu wanaoweza kukusaidia,”.
Kwa mujibu wa taarifa yake iliyotolewa Julai 15 ,2025 na Mkuu huyo wa Takukuru Mkoani hapa wakati akizungumza na watia nia wa ubunge kupitia CCM kutoka Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chama hicho alisema:
"Tumepokea malalamiko 11 katika ofisi yetu ya Takukuru, yanayohusiana na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watiania ya ubunge ndani ya CCM, tunaendelea kuyafanyia kazi na kuyachakata ili tuone ukweli wa malalamiko hayo," alisema Chaulo.
Aliongeza kuwa; "Tumeanza kuyachakata malalamiko hayo ili kubaini ukweli. Kipindi hiki cha uchaguzi malalamiko mengine ni ya watu kutengenezeana tuhuma ambazo sizo sahihi, lakini tupo makini katika kuhakikisha kila tuhuma tunayoipata tunaifanyia kazi kwa undani zaidi ili tuweze kupata uthibitisho.
Hatima ya watia nia wa ubunge na viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado haijulikani, huku macho yakielekezwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kitakachofanya uteuzi Agosti 22.
Mwisho.
Comments
Post a Comment