MAMA LISHE, BABA LISHE 250 WAKABIDHIWA MITUNGI YA GESI TABORA

MAMA LISHE, BABA LISHE 250 WAKABIDHIWA MITUNGI YA GESI TABORA.

Na Musa Mathias. 

Tabora, Tanzania.

Mama lishe na babalishe 250 wilayani Tabora wamekabidhiwa mitungi ya gesi 250 kwa ajili ya matumizi ya nishati safi, katika jitihada za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mitungi hiyo imetolewa na wadau wa maendeleo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Mitungi hiyo imekabidhiwa rasmi leo, Agosti 7, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo B. Wella, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Anglikana karibu na Chuo cha Walimu Tabora (TTC). Hafla hiyo imehusisha wadau mbalimbali wakiwemo Shirika lisilo la Kiserikali la Tabora Integrated Women Organization (TIWO) pamoja na Kampuni ya Tumbaku ya Japan Tobacco International (JTI).



Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bi. Upendo Wella ameishukuru TIWO na JTI kwa mchango wao mkubwa wa kuwezesha upatikanaji wa mitungi hiyo kwa mama lishe na baba lishe, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kuhakikisha jamii inatumia nishati safi.

"Tunapenda kuwapongeza na kuwashukuru wadau wetu, TIWO na JTI, kwa kuona umuhimu wa kusaidia kundi hili muhimu katika jamii yetu. Serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo mkubwa katika matumizi ya nishati safi, na jitihada hizi ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali," aalisema Bi. Upendo Wella.

Ameongeza kuwa lengo la kugawa mitungi hiyo ya gesi ni kuwawezesha mama lishe na baba lishe kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo si rafiki kwa mazingira, akiwataka wanufaika kutumia mitungi hiyo kwa uadilifu na kuepuka kuiuza.

Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mpango huo, akiwemo Bw. Juma Upepo na Bi. Mwajuma Funga, wameishukuru serikali pamoja na wadau waliowezesha upatikanaji wa mitungi hiyo. Wamesema kuwa hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi na wameahidi kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa.

Mtendaji Mkuu wa Shirika la TIWO, Bi. Edith Mkwama, ameishukuru kampuni ya JTI kwa kufanikisha upatikanaji wa mitungi hiyo 250, na kutoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kushirikiana na shirika hilo katika miradi ya kijamii kama sehemu ya kurudisha kwa jamii kupitia programu za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR).

Matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu, uchafuzi wa hewa, na kusababisha matatizo ya kiafya kama vile kikohozi sugu, pumu na matatizo ya mapafu, hasa kwa wanawake na watoto wanaokaa karibu na majiko ya moshi mzito.
























Mwisho.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO