SAMWASA YAIMARISHA USALAMA WA SAME NA MWANGA KWA KUFUNGA 'FIRE HYDRANTS' KWA AJILI YA DHARURA ZA MAOKOZI.

SAMWASA YAIMARISHA USALAMA WA SAME NA MWANGA KWA KUFUNGA 'FIRE HYDRANTS' KWA AJILI YA DHARURA ZA MAOKOZI.

Na Musa Mathias
Kilimanjaro.

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same–Mwanga (SAMWASA) imechukua hatua madhubuti ya kuimarisha usalama wa jamii kwa kufunga mifumo ya kisasa ya maji ya dharura (Fire Hydrants) katika maeneo ya kimkakati wilayani Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Uwekaji wa miundombinu hiyo ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa kurahisisha kazi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuhakikisha magari ya zimamoto yanapata maji kwa haraka na kwa urahisi pindi majanga ya moto yanapotokea, tofauti na hali ya awali ambapo hakukuwa na vituo hivyo.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SAMWASA, Mhandisi Rashid Shaban, amesema uamuzi wa kufunga Fire Hydrants umejikita katika kulinda maisha na mali za wananchi ambao wamekuwa wakihudumiwa na mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, akibainisha kuwa uwepo wa vituo hivyo utawezesha huduma za uokoaji kuwa za wakati na kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya maji ni jibu la moja kwa moja kwa changamoto za kiutendaji zilizokuwa zikilikabili Jeshi la Zimamoto katika ukanda wa barabara kuu ya Dar es Salaam - Kilimanjaro hasa katika wilaya za Same na Mwanga, Same ni moja ya eneo ambalo limekuwa likishuhudia matukio ya dharura mara kwa mara.
Kumbukumbu ya tukio la kusikitisha la Juni 28, 2025, katika eneo la Sabasaba wilayani Same, bado ipo hai baada ya mabasi mawili kugongana na kusababisha mlipuko wa moto uliosababisha vifo takribani 42 na majeruhi. Tukio hilo lililoibua simanzi kubwa kitaifa, lilionesha kwa wazi uhitaji wa vituo vya kudumu vya kuzima moto pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika ili kukabiliana na majanga kama hayo kwa ufanisi.
Katika hatua ya kuimarisha uwezo wa uokoaji, Serikali mnamo Desemba 5, 2025, ilikabidhi gari jipya na la kisasa la Zimamoto na Uokoaji kwa Wilaya ya Same. Hafla ya makabidhiano iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliyemkabidhi gari hilo Mkuu wa Wilaya ya Same huku akisisitiza umuhimu wa kulitunza na kulihifadhi gari hilo kwa uangalifu mkubwa.

Alibainisha kuwa gari hilo ni ukombozi kwa wananchi wa Same, hivyo ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha linabaki katika hali nzuri ya kiutendaji kwa manufaa ya jamii ambapo Mkuu wa Wilaya ya Same aliahidi kulisimamia gari hilo kwa weledi na kuwasihi wananchi kutoa taarifa sahihi na za haraka pindi dharura zinapotokea ili kurahisisha kazi ya vyombo vya uokoaji.

Kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano wa taasisi, SAMWASA imeamua kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuweka miundombinu ya maji itakayorahisisha utekelezaji wa majukumu yao. Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na uongozi wa Kata ya Same pamoja na wananchi kwa ujumla, ambao hapo awali walishuhudia madhara makubwa ya moto kutokana na ukosefu wa maji na vifaa stahiki.

Mamlaka hiyo imetoa wito kwa wananchi kutambua kuwa wao ndio walinzi wa kwanza wa miundombinu ya maji na uokoaji iliyowekwa. Imeelezwa kuwa utunzaji wa vituo vya Fire Hydrants ni jukumu la kila mkazi, kwani kuharibu au kuingilia miundombinu hiyo ni kuhatarisha usalama wa jamii nzima.

Wananchi wamehimizwa kulinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kutoa msaada uliokusudiwa wakati wa majanga, na hivyo kuokoa maisha na mali za watu wa Same na Mwanga. Hatua hii inaashiria mwanzo mpya wa usalama wa majanga ya moto katika ukanda wa Same na Mwanga, ambapo ushirikiano wa taasisi na wananchi unatarajiwa kuokoa maisha na mali.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO