NEEMA YA AFYA NA UJUZI MWANGA: DC RUKIA AFANYA ZIARA YA KISHINDO HOSPITALI YA WILAYA NA VETA.

NEEMA YA AFYA NA UJUZI MWANGA: DC RUKIA AFANYA ZIARA YA KISHINDO HOSPITALI YA WILAYA NA VETA.

Na Musa Mathias, 
Mwanga, Kilimanjaro. 


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Rukia Zuberi,  ametembelea miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pamoja na Chuo cha Ufundi (VETA) ambapo amewasisitiza wasimamizi na mafundi kuhakikisha kazi hiyo inazingatia viwango, ubora na ufundi unaotakiwa ili kuendana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

​Mhe. Rukia ameyasema hayo leo, Februari 06, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi wilayani humo akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya.
Akikagua mradi wa ujenzi wa hospitali, Mhe. Rukia amesema kuwa kukamilika kwa hospitali hiyo kutakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Mwanga katika kuondokana na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa nje ya wilaya.

Amesema hali hiyo awali iliwasababishia wananchi usumbufu, gharama kubwa na kupoteza muda mwingi ambao ungetumika katika shughuli za uzalishaji mali.
Akiwa katika mradi wa Chuo cha VETA, Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa chuo hicho kitakuwa silaha muhimu ya kuwajengea vijana ujuzi na stadi mbalimbali za kazi zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kukabiliana na changamoto ya ajira ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

​Amesisitiza kuwa ujenzi wa miradi hiyo ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo yao.

Aidha, amewataka wasimamizi kutobabaisha na badala yake wakamilishe ujenzi huo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na matunda hayo ya maendeleo yanayolenga kuboresha maisha ya kila mwana-Mwanga.






















Mwisho. 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO