WAZIRI KAIRUKI: SERIKALI KUJENGA USHIRIKIANO IMARA NA SEKTA BINAFSI KUKUZA UCHUMI WA KIDIJITALI




Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mtumba, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angela Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameongoza kikao kazi kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Februari 26, 2026.

Kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema Wizara inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Anga za Juu, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa Februari 8, 2022, kuhusu Serikali kumiliki satelaiti yake kwa ajili ya kutatua changamoto za mawasiliano nchini.

“Ni matarajio yetu kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi, programu hii itachangia kukuza uchumi wa kidijitali na maendeleo ya Taifa kwa ujumla,” amesema Waziri Kairuki.

Aidha, Waziri Kairuki amebainisha kuwa Wizara inaendelea kuimarisha ulinzi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA (CII) kwa kuzingatia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ambapo mwongozo wa kutangaza miundombinu hiyo uko katika hatua za mwisho za uridhiwaji.

Ametoa wito kwa wadau wa sekta kushirikiana na Wizara kulinda na kuendeleza miundombinu hiyo kwa manufaa ya Taifa, akisisitiza kuwa ni jukumu la pamoja kuhakikisha usalama na uimara wake.

Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali, akisema ushirikiano huo ni chachu ya ubunifu, uwekezaji na ajira. Pia ameeleza kuwa Wizara inashirikiana na wadau kuandaa Akaunti ya Upimaji wa Uchumi wa Kidijitali (DESA) ili kubaini mchango wa sekta ya TEHAMA katika pato la Taifa.

Amehimiza watoa huduma za mawasiliano kutumia miundombinu ya pamoja (Co-location) na mfumo wa National Roaming ili kuongeza upatikanaji wa huduma na kuepuka urudufu wa rasilimali.

“Kwa umoja wetu, tuelekeze nguvu kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 hakuna sehemu itakayokosa mawasiliano (‘Zero Spot’). Nina imani tutafanikiwa kwa kishindo,” amesema Waziri Kairuki.

Waziri pia ameeleza kuwa Wizara inaandaa Mwongozo wa Ujenzi Nadhifu wa Miundombinu ya Mawasiliano ili kuhakikisha ujenzi unazingatia ubora, usalama na matumizi ya pamoja.

Aidha, ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Wizara katika kufanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa mfano wa mji wa kisasa unaotumia TEHAMA (Smart City), akisema ni fursa ya kihistoria kwa Tanzania kuonesha uwezo wake katika teknolojia bunifu.

Akihitimisha kikao hicho, Waziri Kairuki amesisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari kwa kushirikiana na sekta binafsi, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu.

“Ni jukumu letu sote kuhakikisha sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari inakuwa nguzo ya maendeleo ya Taifa letu — salama, bunifu, na endelevu,” amesema Waziri Kairuki.





Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO