UWAJIBIKAJI NA USIMAMIZI MADHUBUTI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA UJENZI WA MADARASA.
UWAJIBIKAJI NA USIMAMIZI MADHUBUTI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA UJENZI WA MADARASA.
Na Mwandishi Wetu.
Tunduru.
Jimbo la Tunduru Kusini imekuja na mfumo mpya wa matumizi ya Mfuko wa Jimbo baada ya kupitisha Shilingi milioni 65.9 kwa mkakati maalum wa kutatua changamoto ya madarasa, tofauti na utaratibu wa awali wa kugawa fedha kidogo kidogo katika miradi mingi isiyoonekana matokeo yake kwa wananchi.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Mfuko wa Jimbo kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhandisi Fadhili Chilombe.
Kwa mujibu wa maazimio ya kikao hicho, zaidi ya mifuko 1,800 ya saruji itanunuliwa kwa ajili ya kufyatua tofali yatakayotumika kujenga madarasa katika shule mbalimbali za jimbo hilo. Lengo ni kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa vyumba vya madarasa na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akizungumza katika mahojiano baada ya kikao hicho,Mhandisi Fadhili Chilombe alieleza kuwa huu ni mfumo mpya kabisa ambao haujawahi kutekelezwa na watangulizi wake katika Jimbo la Tunduru Kusini.
Alibainisha kuwa kwa muda mrefu fedha za Mfuko wa Jimbo zilikuwa zikigawanywa katika miradi mingi kwa kiwango kidogo, hali iliyosababisha kutokuonekana kwa matokeo yenye athari kubwa kwa wananchi wa kawaida.
“Badala ya fedha kusambazwa kidogo kidogo bila kuacha alama, sasa tunaelekeza nguvu katika eneo moja lenye uhitaji mkubwa ili matokeo yake yaonekane wazi na yawe ya kudumu,” alisema.
Aliongeza kuwa mpango huo umewekwa kwa mtazamo wa miaka mitano, ukilenga kumaliza changamoto ya miundombinu ya madarasa katika shule za jimbo hilo, badala ya kuendelea na miradi midogo midogo isiyotoa suluhisho la kudumu.
Wajumbe wa kamati walisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti katika ununuzi wa saruji, ufundi wa kufyatua tofali na utekelezaji wa ujenzi, wakieleza kuwa uwajibikaji na mawasiliano ya karibu vitakuwa msingi wa mafanikio ya mkakati huo mpya wa maendeleo.







Comments
Post a Comment