UHAMIAJI SIHA WATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA ZA WAGENI WASIOFAHAMIKA
Siha, Kilimanjaro. Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Siha imewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wageni wasiowafahamu katika maeneo yao ili kurahisisha ukaguzi na kudhibiti uhamiaji usiohalali. Wito huo umetolewa jana na Mratibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Ombeni Ndeliso Shuma, wakati akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake.
Mratibu Shuma amesema kampeni ya “Mjue Jirani Yako” inayotekelezwa nchini kote inalenga kuwahimiza wananchi kutambua watu wanaoishi au kufika katika maeneo yao, hususan wale wageni ambao hawajulikani. Amesema kutoa taarifa za mapema kunawapa uhamiaji nafasi ya kufanya ukaguzi ili kubaini kama wahusika wana vibali halali vya kuwepo nchini.
Akifafanua, Shuma amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu watu wanaowazunguka kwa ajili ya usalama wao na wa jamii. “Kama kuna mgeni hamjawahi kumuona, toa taarifa haraka. Ni jukumu letu kufika, kukagua na kuthibitisha kama yupo kihalali au la,” amesema.
Aidha, amesema Uhamiaji Wilaya ya Siha inaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo masoko ya Lawate na Sanya Juu ili kuongeza uelewa kuhusu kampeni hiyo. Elimu hiyo inawasaidia wananchi kutambua viashiria vya uwepo usio rasmi wa wageni katika jamii.
Shuma ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama ni msingi muhimu katika kulinda amani ya wilaya hiyo. Amesema idara yake itaendelea na ukaguzi, doria na utoaji elimu mara kwa mara kuhakikisha Siha inabaki kuwa eneo salama kwa wote.

Comments
Post a Comment