VIJANA MTWARA WATAKA FURSA
Na. OR – MV, Mtwara
Vijana wa mkoa wa Mtwara wamesema wanahitaji Serikali iwasaidie kuweka mazingira wezeshi ili fursa za kiuchumi zilizopo ziwasaidie kuzalisha ajira na kudumisha amani ikiwa ni matunda ya kuanzishwa wizara ya vijana kwa mara ya kwanza nchini.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati na vijana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana na mbunge wa Mtwara Mjini Joel Nanauka (29 Novemba 2025) mjini Mtwara alisema Serikali itatumia muda mwingi kutafuta fursa za maendeleo kwa vijana badala ya kudhibiti vijana.
Waziri wa Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka aliwaeleza vijana kuwa dhmaira ya kuundwa wizara hiyo ni kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona mawazo na fikra za vijana nchini zinasikika ili kutatua changamoto zao.
Nanauka aliongeza kusema katika kuhakikisha vijana wanapata mitaji na kuwa na uhakika wa kipato amekusidia kuanzisha mfuko maalum wa vijana (Saccos) waendesha pikipiki na akina mama wajasiliamali ambapo atachangia mfuko uwe na uwezo wa kukopesha vijana itakayowasaidia kuwa na uhakika wa ajira.
Nanauka amewataka vijana wa mkoa wa Mtwara kuitunza amani na kwamba kama alivyoahidi wakati wa uchaguzi, ataendelea kuwa mtumishi wa wote kwa maendeleo ya wote ambapo amewataka vijana wenye mawazo ya ubunifu wa biashara kuwasiliana na ofisi yake ili utaratibu wa kuwasaidia kuboresha mawazo hayo kuwa biashara ufanyike.
Vijana wakizungumza kwenye ziara hiyo akiwemo Hamza Kalinga mkazi wa kijiwe cha kahawa cha Chilindima alisema vijana wa Mtwara hawahitaji maandamano kwa kuwa hata baaada ya uchaguzi mkuu uliopita hawakushiriki kwenye vurugu badala yake mahitaji yao ni fedha za kuanzisha biashara.
Akiwa katika Stendi ya mabasi ya Mkanaledi Waziri Nanauka alizungumza na vijana ambapo Hussein Said alisema kwa hali ilivyo nchini kwa sasa vijana hawaoni sababu ya kuandamana tena kuchochea ugomvi bali kuhakikisha wanashirikiana na serikali kuibua fursa na kutatua changamoto ikiwemo ukosefu wa mitaji.
Kwa upande wake Tabu Mashaka alimpongeza Waziri wa Vijana kwa uamuzi wake wa kuzunguka mikoani kuzungumza na vijana ambapo amemtaka afikishe salamu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kushukuru kwa kuunda wizara ya vijana ili itatue kero.
Nikuombe Waziri kazunguke mikoani, hakuna atakayechokozeka, vijana tuna wizara ya kusemea .Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia wizara hii na kwamba tunakuomba uitendee haki ili maslahi ya vijana yapate kipaumbele” alisema Tabu.
Hata hivyo, kijana Anjira Mussa wa mtaa wa Chilindima alimweleza Waziri huyo kero wanayoipata vijana waendesha pikpiki toka kwa askari Polisi hatua inayowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao na kuomba mahusiano ya jeshi hilo na raia yaboreshwe.
Waziri Nanauka yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya kukutana na vijana na kusikiliza maoni na mawazo yao kuhusu Tanzania wataitakayo ambapo leo ametembelea mtaa wa Mdenga, Muungano -Chilindima, stendi ya Mkanaledi na stendi ya Mikindani akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Kedmon Mapama pamoja na viongozi wa Mkoa.





Comments
Post a Comment