JAMII YAASWA KUSIMAMA NA KUWAJALI WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

JAMII YAASWA KUSIMAMA NA KUWAJALI WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM


Na Musa Mathias. 
Same, Kilimanjaro. 

Katika jamii ambayo mara nyingi imekuwa ikisahau au kupuuza mahitaji ya watoto wenye uhitaji maalum, wito umetolewa kwa kila mmoja kusimama na kuwa sehemu ya mabadiliko—kwa kuwatia moyo, kuwajali na kuwapa fursa sawa ya kuishi maisha yenye heshima, matumaini na ndoto zinazoweza kutimia kama ilivyo kwa watoto wengine.

Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali wakati wa hafla ya Iftar Gala iliyoandaliwa na Benki ya NMB tawi la Same kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Same na kuwakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini pamoja na jamii kwa ujumla katika kuonesha mshikamano kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Same, Sheikh Iddy Jumaa, amesema kuwa jukumu la kuwasaidia watoto hao si la serikali pekee bali ni la kila mwanajamii, akisisitiza kuwa upendo, kujali na msaada wa pamoja vinaweza kubadilisha maisha yao na kuwapa nafasi ya kufikia mafanikio.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Same, Bi. Mamndolwa Gembe, ameeleza kuwa malezi bora yenye upendo na uangalizi ni msingi muhimu katika kuwajengea watoto hao kujiamini, huku akihimiza jamii kubadili mtazamo hasi na badala yake kuwaunga mkono ili waweze kukua katika mazingira salama na yenye fursa sawa.
Akitoa taarifa ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Msingi Same, Faustine Richard, amesema kuwa shule ina wanafunzi 45 wenye mahitaji maalum, wakiwemo wavulana 26 na wasichana 19, ambapo baadhi yao ni wasioona, wenye uoni hafifu pamoja na wenye ulemavu wa ngozi, hali inayohitaji uangalizi na msaada wa karibu katika kujifunza.

Ameongeza kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na walimu, bado kuna changamoto za uhaba wa vifaa maalum vya kujifunzia pamoja na mahitaji mengine ya msingi, hivyo kuna umuhimu wa wadau na jamii kuendelea kushirikiana katika kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto hao.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya NMB tawi la Same, Bw. Saad Masawila, amesema kuwa wameamua kushiriki futari na watoto hao ikiwa ni sehemu ya kuonesha upendo na mshikamano, huku wakitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia mahitaji mbalimbali kuelekea sikukuu za Iddi na Pasaka.

Hafla hiyo imeambatana na utoaji wa misaada mbalimbali na kutoa ujumbe mzito kwa jamii kuwa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum si hisani bali ni wajibu wa pamoja, huku ikihimiza kuondoa unyanyapaa na kujenga jamii yenye upendo, usawa na matumaini kwa kila mtoto.














Mwisho.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO