SERIKALI YAHARAKISHA MIKAKATI KUIMARISHA UPATIKANAJI MAFUTA
SERIKALI YAHARAKISHA MIKAKATI KUIMARISHA UPATIKANAJI MAFUTA
Na Mwandishi Wetu.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Mwainyekule leo ameshiriki kikao cha ngazi ya juu cha wamiliki wa kampuni za uuzaji wa bidhaa za mafuta aina ya petroli (OMCs) kilichoitishwa na Waziri wa Nishati Deogratias Ndejembi, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini.
Kikao hicho kimekuja katika kipindi ambacho dunia inashuhudia mvutano wa kisiasa na kiusalama kati ya Iran na United States, hali inayoweza kuathiri mnyororo wa usambazaji wa mafuta katika masoko ya kimataifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Ndejembi aliwahakikishia wadau hao ushirikiano thabiti wa Serikali na kusisitiza kuwa hatua stahiki zimechukuliwa kukabiliana na athari zozote zinazoweza kujitokeza.
“Serikali iko macho, imejipanga na imefanya kila linalowezekana kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa mafuta, na tutawapatia ushirikiano wa hali ya juu. Ni rai yangu kwa kila mmoja kufuata sheria za nchi,” amesema.
Aidha, aliwataka wamiliki wa kampuni za mafuta kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa Watanzania bila vikwazo, huku wakizingatia taratibu na sheria zilizowekwa.
Kwa upande wake, Dkt. Mwainyekule alisisitiza kuwa mamlaka itaendelea kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wote wanaofuata utaratibu, na kuonya kuwa yeyote atakayekiuka masharti au kuhujumu upatikanaji wa mafuta atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Hatua hizi zinatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kulinda uthabiti wa sekta ya nishati na kuhakikisha wananchi hawapati athari za moja kwa moja kutokana na misukosuko ya kimataifa.






Comments
Post a Comment