VIJANA 2,550 WAWEZESHWA AJIRA SEKTA YA MADINI KUPITIA MRADI WA MBT.
VIJANA 2,550 WAWEZESHWA AJIRA SEKTA YA MADINI KUPITIA MRADI WA MBT.
Na Deborah Lemmubi
Dodoma.
Katika kuhakikisha ushiriki wa vijana unaongezeka katika Sekta ya Madini kwenye eneo la utafutaji,uchimbaji na biashara ya madini hayo, Tume ya Madini kupitia mradi wa Mining for Better Tomorrow imetoa leseni 273 kwa vikundi 183 vya vijana ambavyo husajiliwa kwenye Halmashauri zao.
Ambapo leseni hizo zilitolewa katika Mikoa ya Kimadini ya Mara,Mtwara,Dodoma,Mirerani na maeneo mengine ambazo zinajumuisha uchimbaji wa madini ya dhahabu,shaba,madini ya vito,madini ya viwandani na madini ya ujenzi ambapo hadi kufikia Disemba 2025 vijana 2,550 wamewezeshwa kupata ajira za moja kwa moja kupitia mradi huo wa MBT.
Hayo yameelezwa mapema leo hii Jijini Dodoma Machi 16,2026 na Mkurugenzi wa Ukagizi wa Migodi na Mazingira Mhandisi Hamisi Kamando akimwakikisha Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akielezea fursa za vijana zilizopo katika Sekta hiyo ya Madini.
"Sekta ya Madini imeendela kuhakikisha inaongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2025 Tume ya Madini kupitia mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (Mining for Better Tomorrow) (MBT) imetoa leseni 273 kwa vikundi 183 ya vijana ambavyo husajiliwa kwenye Halmashauri zao".
"Leseni hizo zilitolewa katika Mikoa ya Kimadini ya Mara, Mbogwe, Kagera, Shinyanga, Morogoro, Rukwa, Dodoma, Mtwara, Singida, Njombe na Mirerani. Miradi ambayo leseni hizo zimetolewa zinajumuisha uchimbaji wa madini ya dhahabu, shaba, madini ya vito, madini ya viwandani ya chumvi pamoja na madini ya ujenzi. Hadi kufikia Desemba, 2025 Tume ya Madini imewezesha vijana 2,550 kupata ajira za moja kwa moja kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (MBT)".
Aidha Mhandisi Kamando amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume hiyo imeendelea kutenga maeneo ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini ili kwa pamoja waweze kufaidika na rasilimali ambazo nchi imejaaliwa na maeneo yanayotengwa na kugawiwa kwa wananchi sehemu kubwa yanawalenga vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 45.
Ambapo hadi sasa jumla ya maeneo 65 yamependekezwa kutengwa kwa ajili ya kugawiwa kwa Wachimbaji Wadogo katika mikoa ile ile ya kimadini ya Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani, Tanga, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya na Ruvuma.
Ikiwa ni pamoja na Wizara kuendelea kutoa kipaumbele katika utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo, ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2025 Serikali imetoa jumla ya leseni 5,983 sawa na asilimia 71 ya leseni zote zilizotolewa katika kipindi husika ma Leseni za uchimbaji mdogo wa madini hutolewa kwa Watanzania pekee ambao sehemu kubwa zimeombwa na kundi la vijana wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 45.
Pia ameeleza kuwa katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na Tume ya Madini kuweza kuwahudumia Watanzania kwa wakati na kwa viwango, katika bajeti ya Mwaka 2025/2026 Tume kupitia Wizara ya Madini imetengewa bajeti ya jumla ya Shilingi 25,335,000,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo fedha hizi zimelenga kuimarisha utendaji kazi wa Tume ya Madini katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa Wananchi wote.
Ambapo fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vitendea kazi kama vile magari, mashine za utambuzi wa madini ya metali (XRF) zitakazotumiwa na watalaam katika kutoa huduma kwa wananchi kwenye masoko ya madini na baadhi ya migodi mikubwa, ya kati na midogo ya madini nchini, Ujenzi wa majengo ya ofisi za madini nchini na ununuzi wa samani ili kuweka mazingira bora kwa watumishi katika kutoa huduma kwa watanzania,sambamba na kugharamia mafunzo maalum ya kitaalam kwa watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini ambayo iliundwa na Sheria ya Madini Sura 123 na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 17 Aprili, 2018.
Mwisho.



Comments
Post a Comment