MRADI WA DMDP II KUJENGA KILOMITA 42.78 ZA LAMI KIGAMBONI



Dar es Salaam 

Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara Kilomita 42.78 kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) katika kata za Mjimwema, Kibada, Kigamboni, Vijibweni na Somangila zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Edgar Tumsifu ambapo amesema kuwa mradi huo unaogharimu shilingi Bilioni 110 utekelezaji wake umefikia asilimia 30 huku tayari umeshaanza kuleta matokeo kwani barabara zilizokuwa na changamoto zimeshaanza kufanyiwa kazi na zikikamilika wananchi watanufaika na miundombinu hiyo.

"Tunaishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu, TARURA Kigamboni tuna mtandao wa barabara Km 1035 kati ya hizo barabara za lami ni Km 10 lakini kupitia DMDP II imetuletea Km 42.78 kwahiyo tutakuwa na zaidi ya Km 50 za barabara za lami mpaka kufikia mwezi Agosti mwaka huu", amesema.

Ameeleza kuwa barabara hizo zikikamilika zitasaidia kupunguza uharibifu wa vyombo vya usafiri, pia kuna baadhi ya barabara ambazo ni 'bypass' zikikamilika zitasaidia wakazi wa Kigamboni wanaoelekea maeneo ya Kivukoni au darajani kufika kwa urahisi na haraka. 

"Leo tumetembelea barabara zenye urefu wa Km 10.48 zilizopo kata ya Kibada ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 68, mkandarasi anaendelea na ujenzi wa mitaro na njia za waenda kwa miguu, barabara hizi zikikamilika zitasaidia kupunguza foleni katika maeneo haya", amesema.

Amesema kazi zitakazofanyika katika mradi wa DMDP II ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, njia za waenda kwa miguu, vituo vya daladala, taa za barabarani na mifereji ya maji ya mvua zaidi ya Km 80.

Aidha, amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi cha mpito cha ujenzi mara baada ya shughuli za ujenzi kukamilika mitaa yote itapendeza na kuwa safi na salama na pia wawe walinzi wa miundombinu hiyo wasitupe taka kwenye mitaro wala wasipitishe magari yenye uzito mkubwa.

Naye, Mwenyekiti wa mtaa wa Kichangani kata ya Kibada, Bw. Nassoro Chande amesema ubovu wa barabara uliokuwepo awali ulikwamisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii lakini kwa sasa hali ya kiuchumi itaimarika kufuatia kuendelea kwa ujenzi wa barabara hizo ambazo kwa sasa watu wengi wanajenga maeneo hayo na kufanya thamani ya ardhi kupanda.

Bw. Frank Mwakipageme ambaye ni mfanyabiashara eneo la Shangwe kata ya Kibada amesema kuwa adha kubwa waliyokuwa wanaipata ni maji kujaa hasa kipindi cha mvua kwasababu eneo hilo kuna bonde lakini sasa wamepata nafuu baada ya kutengenezewa mitaro na wanafanya biashara zao bila shida na ameiomba serikali iendelee kuwaboreshea miundombinu ili kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi. 

Bw. Albano Nditi mkazi wa mtaa wa Kiziza ameishukuru serikali kwa kuwaboreshea miundombinu na ameomba waongezewe alama za barabarani na matuta na pia ameomba wananchi wenzake wailinde miundombinu hiyo kwa kuwa wastaarabu na kutotupa takataka kwenye mifereji.





 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO