*MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA SHIRIKA LA KIINJILI LA KIMISHENI DUNIANI*
_*ASISISTIZA UMUHIMU WA KANISA NA SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI*
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wa mashirika yote ya kidini kuendelea kufanya kazi pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali ili kuweza kuwatumikia vema wananchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Kiinjilisti la Kimisheni Duniani (UEM) uliofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam. Amesema ni vema Serikali na mashirika ya kidini kushirikiana zaidi katika kukabiliana na theolojia potofu, kukabiliana na umasikini, uharibifu wa mazingira pamoja na changamoto zinazojitokeza baina ya dini.
Pia Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania, itaendelea kusimamia haki ya kuabudu na ya kiroho kwa watu wote na kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kufurahia amani na utulivu.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa washiriki wa mkutano huo kujadili changamoto mbalimbali zinazoikumba Dunia kama vile hitaji la kulinda, kuhifadhi bioanuwai na kutumia mazingira kwa njia endelevu si kwa manufaa ya wachache tu bali kwa manufaa ya wanadamu wote, mimea na Wanyama. Amesema ripoti za kisayansi zinaonyesha kuwa maisha ya mwanadamu yatapungua ifikapo mwaka 2030 ikiwa uharibifu mkubwa wa rasilimali za Dunia na athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira hazitadhibitiwa, kama jambo la dharura.
Vilevile, Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa Mkutano huo na Kanisa kwa ujumla kufanya uwekezaji makini katika miradi muhimu ya utoaji huduma za kijamii ili kuongeza manufaa ya uwekezaji huo na kupunguza utegemezi kwa wafadhili.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amelipongeza Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa kwa kazi kubwa linayofanya katika kusaidia watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu. Amesema matokeo ya kazi hiyo yamepelekea kuboresha maisha kwa watoto wenye ulemavu na watu binafsi wenye ulemavu wa afya ya akili, na hivyo kukuza ushirikishwaji zaidi wa kundi hilo. Amelihimiza Kanisa kuongeza zaidi utoaji huduma kwa watu wenye mahitaji maalum kwa kuwa bado jamii inahitaji huduma hizo.
Mkutano huo unachagizwa na Kauli mbiu isemayo "Boriti Katika Jicho Letu: Ubaguzi Kanisani na Udiakonia" una lengo la kutathmini maisha ya wanadamu, kuthamini utu wa binadamu na kuondoa mitazamo ya kibaguzi pamoja na vizuizi vya kimfumo kwa makundi mbalimbali. Mkutano huo unashirikisha wajumbe kutoka Bara la Ulaya, Afrika pamoja na Asia.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
14 Septemba 2025
Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment