DC RUKIA AANZA ZIARA KATA KWA KATA, AHIMIZA UWAJIBIKAJI.
DC RUKIA AANZA ZIARA KATA KWA KATA, AHIMIZA UWAJIBIKAJI.
Mwanga, Kilimanjaro.
Katika hatua ya kusogeza huduma za Serikali karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapata majibu kwa wakati, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bi. Rukia Zuberi, amewataka viongozi ngazi za kata, vijiji na vitongoji na watumishi wa umma ngazi zote wilayani humo kuacha utendaji wa kusubiri taarifa maofisini na badala yake kuwafikia wananchi katika maeneo yao, kusikiliza kero zao na kuchukua hatua za kuzitatua.
Akizungumza na watumishi wa umma, wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na madiwani katika kikao kilichofanyika Shule ya Msingi Kivindu, Tarafa ya Usangi, Bi. Rukia amesema dhamana waliyopewa na Serikali inapaswa kuonekana kupitia utendaji wenye matokeo na huduma zinazogusa maisha ya wananchi.
Bi. Rukia kabla ya kuzungumza na viongozi wa ngazi za kata, vijiji na vitongoji alitembelea na kuzungumza na maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda ambapo alisisitiza zaidi suala la usalama, nidhamu na matumizi sahihi ya shughuli hiyo, akiwataka kuepuka kushawishiwa au kutumiwa katika vitendo vya uhalifu na shughuli nyingine zinazoweza kuhatarisha usalama wao na jamii.
Amewataka vijana hao kutumia bodaboda kama fursa ya kujipatia kipato kwa njia halali na kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanapokutana na viashiria vya uhalifu.
Katika eneo la Soko la Kirongwe, Usangi, Mkuu huyo wa Wilaya alijionea shughuli za wafanyabiashara na hali ya mazingira ya soko hilo, huku akieleza kuwa masoko ni sehemu muhimu ya kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi, hivyo yanapaswa kusimamiwa kwa ufanisi.
Ziara hiyo imeendelea kusisitiza dhamira ya Serikali ya kupeleka huduma na utatuzi wa changamoto karibu na wananchi, huku viongozi wa ngazi za kata, vijiji na vitongoji wakitakiwa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kusimamia kwa vitendo masuala yanayogusa maisha na maendeleo ya wananchi.
Imeandaliwa na musamathiasnjogolo
Email. musamathiasnjogolo@gmail.com
Kilimanjaro, Tanzania.






Comments
Post a Comment