MWANAFUNZI WA DARASA LA PILI AOZESHWA SAME, MUME ATIWA MBARONI, DC KASILDA AAHIDI KISASI CHA KISHERIA
MWANAFUNZI WA DARASA LA PILI AOZESHWA SAME, MUME ATIWA MBARONI, DC KASILDA AAHIDI KISASI CHA KISHERIA
Na Musa Mathias
Same, Kilimanjaro.
Serikali ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kumuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina limehifadhiwa, ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Jiungeni, iliyopo Kata ya Ruvu wilayani humo baada ya kubainika kuwa familia yake ilimkatisha masomo na kumpeleka kwa mwanaume kwa lengo la kumuozesha.
Akizungumza leo Agosti 11, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema Serikali ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu mtoto huyo kuozeshwa, ambapo alituma maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi na walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 kama Mume na Mke.
“Serikali inalaani vikali kitendo hiki cha kikatili cha kumnyima mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu na kukua katika mazingira salama, mpaka sasa watuhumiwa tayari wapo mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria na niwaombe wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kuhusu vitendo vya aina hiyo" Amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, Mhe. Kasilda amesema shule ya Jiungeni ilijengwa mahususi kwa ajili ya kuwakomboa watoto wa jamii ya Kifugaji wanaoishi katika eneo hilo huku akieleza huenda kuna wanafunzi wengine walioacha shule kutokana na ndoa za utotoni au kwenda kuchunga mifugo, akisisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu. Amesema, “Msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni lazima watoto waende shule na sisi tutapambana na wazazi wanaokiuka maelekezo ya Serikali.”
Amepongeza maafisa wa Serikali na wananchi waliofanikisha zoezi la kumwokoa mtoto huyo kwa kushirikiana na wananchi wema, wakifanya uchunguzi katika mazingira magumu ya porini ambako mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana huyo kama mke.
Mhe. Kasilda pia amewaonya baadhi ya watu wanaopanga kutoa rushwa kwa lengo la kuwaachia watuhumiwa akieleza kuwa watakaobainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehatarisha usalama, elimu na ustawi wa watoto.
Imeandaliwa na musamathiasnjogolo
Email musamathiasnjogolo@gmail.com
Mwisho.
#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update
Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX
karibu sana.

Comments
Post a Comment