ZAIDI YA WATU 20 WAHOJIWA SAME KWA TUHUMA ZA UCHIMBAJI HARAMU WA MADINI
ZAIDI YA WATU 20 WAHOJIWA SAME KWA TUHUMA ZA UCHIMBAJI HARAMU WA MADINI
Na Musa Mathias,
Same, Kilimanjaro.
Zaidi ya watu 20 wanahojiwa na Jeshi la Polisi wilayani Same kwa tuhuma za kudaiwa kuendesha shughuli za uchimbaji haramu wa madini katika vyanzo vya maji ndani ya mita 60 kinyume cha sheria na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Akizungumza kuhusu hatua zinazochukuliwa, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema Kamati ya Usalama ya wilaya ilipata taarifa za siri kuhusu uchimbaji huo katika maeneo mbalimbali na kufika kujiridhisha, ambapo ilibaini kuwepo kwa shughuli hizo.
Amesema baada ya kubaini hali hiyo, Kamati iliunda timu ya kwanza ya wataalamu kutoka RUWASA, Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Maafisa Mazingira na Maafisa Madini, iliyofanya uchunguzi katika maeneo yote na kubaini uchimbaji haramu katika kata saba pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Aidha, iliundwa timu ya pili kutoka ndani ya Kamati ya Usalama kwa ajili ya kuwabaini wahusika waliotajwa katika taarifa za siri zilizotolewa na wananchi na baadhi ya madiwani wenye nia njema na wazalendo.
“Hadi sasa zaidi ya watu 20 wanaotuhumiwa kuhusika na uchimbaji huo pamoja na kupeleka mitambo wamehojiwa na Jeshi la Polisi, na wengine wanaendelea kuhojiwa kwa awamu ili kupata ushahidi na watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria, na viongozi wa Serikali watakaobainika pia watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma,” amesema Mhe. Kasilda.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema hali kama hiyo iliwahi kutokea mwaka 2023, ambapo Kamati ya Usalama ilitembelea maeneo hayo na kufanikiwa kuwakamata zaidi ya watu watano waliokuwa wakijihusisha na uchimbaji haramu pamoja na mitambo yao, hali iliyofanya shughuli hizo kusitishwa kwa muda Hata hivyo, amesema uchimbaji huo umeibuka tena mwaka huu na hatua za kuwadhibiti zinaendelea.
Pia, wachimbaji hao wamebainika kufanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na vibali wala leseni kutoka kwenye mamlaka husika huku Mhe. Kasilda akiwaonya watu wanaopanga kurejea katika maeneo hayo na kuendelea na uchimbaji haramu, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaokiuka taratibu.
Mhe. Kasilda amezitaka taasisi za Serikali zinazohusika na uhifadhi wa mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua za kisheria.
Pia amewapongeza wananchi na baadhi ya madiwani waliotoa taarifa za siri na kusisitiza kuwa Serikali itawalinda.
#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update
Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX
karibu sana.






Comments
Post a Comment