EU KUANZISHA KITUO MAALUM CHA MAFUNZO KWA WAKULIMA WA KAHAWA TANZANIA.
EU KUANZISHA KITUO MAALUM CHA MAFUNZO KWA WAKULIMA WA KAHAWA TANZANIA.
Na Mwandishi Wetu.
Moshi, Kilimanjaro.
Umoja wa Ulaya (EU) umetangaza mpango wa kuanzisha kituo maalum cha mafunzo kwa wakulima wadogo wa kahawa nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kuongeza tija, ubora, na ushindani wa zao hilo katika soko la kimataifa.
Mpango huo unalenga kuwajengea uwezo wakulima kupitia mafunzo ya kisasa, matumizi ya teknolojia bora za kilimo, pamoja na usimamizi sahihi wa rasilimali, ili kuongeza uzalishaji wa kahawa bora inayokidhi viwango vya kimataifa, hususan kwa soko la Umoja wa Ulaya na Italia.
Akizungumza katika ziara yake kwenye shamba la kahawa la Kilimanjaro Plantation Limited (KPL), lililoko eneo la Mweka, Wilaya ya Moshi, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Coppola, alisema juhudi hizo ni sehemu ya dhamira ya EU kusaidia wakulima wa Tanzania kupata maarifa na nyenzo zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara ya kimataifa ya kahawa.
"Tutahakikisha wakulima wanapata mafunzo na zana za kuzalisha kahawa yenye ubora wa juu, itakayokuwa na uwezo wa kuingia kwa urahisi kwenye masoko ya Ulaya na Italia," alisema Balozi Coppola.
Balozi huyo aliongeza kuwa ziara yao imewawezesha kujionea kwa macho ubora wa shughuli za kilimo cha kahawa katika shamba la KPL, huku akivutiwa na kazi kubwa inayofanyika na bidhaa bora zinazozalishwa.
"Tumeona shamba zuri, lenye usimamizi mzuri na uzalishaji wenye tija. Hii ni ishara kwamba Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuwa mshindani wa kweli katika soko la kahawa duniani," aliongeza.
Alibainisha kuwa Italia imejipanga kikamilifu kusaidia mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya kahawa Tanzania, ikiwemo kuanzisha kituo cha mafunzo ambacho kitakuwa na jukumu la kuwajengea wakulima wadogo uwezo na ujuzi utakaowawezesha kuongeza ubora wa mazao yao.
"Tunataka kuona wakulima wa Kilimanjaro na maeneo mengine nchini wanazalisha kahawa inayokidhi viwango vya kimataifa na kufikia kwa urahisi masoko ya Ulaya na Italia," alisema Balozi Coppola.
Kwa upande wake, Meneja wa shamba la KPL, Colton Rebenold, alisema kuwa kilimo cha kahawa kimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya kilimo nchini, na kwamba shamba hilo huzalisha kati ya tani 500 hadi 700 za kahawa kila mwaka, ambazo huuza katika masoko ya Ulaya, ikiwemo Italia, na Japan.
"Tuna zaidi ya hekta 620 zenye zaidi ya miti milioni 1.2 ya kahawa. Uzazi huu unatupatia tani nyingi za kahawa kila mwaka, na maganda yanayotokana na usindikaji wake tunayatumia kutengeneza mbolea ya kioevu ambayo huongeza rutuba ya udongo," alisema Rebenold.
Aliongeza kuwa kila wiki mbili hupata lita 400 za mbolea ya kioevu kutoka kwenye maganda ya kahawa, ambayo hupuliziwa kwenye mashamba, na inaweza kutumika kwenye hekari 50.
Aidha, Rebenold alieleza kuwa ujio wa mabalozi kutoka Umoja wa Ulaya ni ishara ya ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Ulaya katika kuimarisha soko la kahawa, jambo linaloongeza hamasa kwa wakulima kuongeza uzalishaji na ubora.
Mwisho.
#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update
Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX
karibu sana.
Comments
Post a Comment