DKT. BITEKO KUFANYA MAKUBWA KATA YA BUGELENGA*
📌 *Asema watakaounganishiwa umeme kupewa majiko*
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewapongeza wananchi wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe kwa kushirikiana na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata yao ikiwemo ujenzi wa shule, barabara na miradi ya maji.
Ametaja moja ya mradi kuwa ni ujenzi barabara ya Bufanka - Ikalanga hadi Bukombe ambapo ameahidi kuwa CCM ikipewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, itatekeleza miradi zaidi ili kuwaletea maendeleo wananchi kwa kukabiliana na kero zinazowakabili.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 20, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Bugelenga wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji sita vya Kata ya Bugelenga na kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika vitongoji tisa vya Kata hiyo.
Amewaeleza wananchi kuwa CCM itaendelea kusogeza huduma bora za jamii ambapo ameahidi kuwa kuanzia sasa wananchi wakiunganisha umeme watapewa majiko ya umeme bure ikiwa ni njia ya kupunguza gharama ya kupikia ikilinganishwa na matumizi ya kuni.
Dkt. Biteko pia amesema watajenga kituo kikubwa cha kupooza umeme ili kuweza kusambaza umeme huo hadi Mbogwe, watajenga madarasa, maabara na jengo la utawala.
“ Mgombea udiwani ameeleza kuhusu shule zinazohitaji ukarabati hivyo ni lazima zikarabatiwe katika kipindi kinachokuja. Pia,
Nataka niwaambie tutajenga wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa katika Kata hii,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM imedhamiria kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuongeza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji.
Kuhusu umuhimu wa elimu, amewaasa wananchi hao kuwasomesha watoto wao kwa kuwa Serikali imeendelea kulipa ada kwa wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita.
Vilevile, amehimiza wananchi wa Bugelenga kumchagua mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa katika kipindi cha uongozi wake amekuwa na mapenzi na wananchi hao kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Bugelenga, Donald Rubigisa amewashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa kushirikiana naye katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga shule.
Amemshukuru Dkt. Biteko kwa kusaidia kujenga daraja kubwa lililoondoa adha ya usafiri kwa wananchi hususan wakati wa masika.
“ Nawashukuru kwa imani yenu kwangu nataka niwaambia mimi nitafanya kazi, mkinichagua mimi, Dkt. Biteko na Dkt. Samia Suluhu Hassan tutatekeleza miradi mipya ya maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amesema Kata yake ina shule zinazohitaji ukarabati ikiwemo Shule za Msingi Bufanka, Bugelenga na Msasani hivyo amemuomba Dkt. Biteko mara atakapo chaguliwa tena kuwa mbunge asaidie kuboresha shule hizo.
Pia, amesema Kata hiyo inahitaji chumba cha kuhifadhia maiti na kukosa mawasiliano ya simu ya uhakika.
Mgombea huyo amewahimiza wananchi wake Oktoba 29 kujitokeza kwa wingi na kuwachagua wagombea wa CCM.
Comments
Post a Comment