MD TWANGE ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA TAZA – AAGIZA KUONGEZWA KWA KASI YA UTEKELEZAJI


📌*Asema  njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 (203 km) Tunduma -Sumbawanga umefikia zaidi ya asilimia 79.07*📌*Amshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye miradi ya umeme*

Na Josephine Maxime, Songwe

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania-Zambia Transmission Interconnector (TAZA), kupitia njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kilovoti 400 (203 km) Tunduma Sumbawanga ambao kwa sasa umefikia zaidi ya  asilimia 79.

Amesema Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa, na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo hayo.

Katika ziara yake Mkoani Songwe na Mbeya Septemba 18, 2025  Bw. Twange amesisitiza umuhimu wa wakandarasi kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, kama ilivyopangwa katika mikataba.


“Kwanza tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha za kutekeleza miradi, kazi hii sio ndogo lakini maendeleo ni mazuri, kwa mfano katika njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, mkandarasi amesema tayari  amesimamisha nguzo 171 kati ya 497  kazi yetu ni kumsimamia amalize kwa wakati ,” alisema Bw. Twange.

Katika kituo cha kupoza umeme cha Malangali, ambacho ni miongoni mwa vituo vitano vinavyotekelezwa chini ya mradi wa TAZA, Bw. Twange alieleza kuwa maendeleo yamefikia asilimia 36. Amemtaka Mhandisi  anayesimamia Mradi kuongeza usimamizi wa karibu kwa mkandarasi.

Bw. Twange ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya umeme, akisisitiza kuwa hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya umeme.

Mbali na mradi wa njia ya kusafirisha umeme Tunduma–Sumbawanga, Mkurugenzi Mtendaji pia alitembelea Kituo cha kupoza umeme cha Iganjo kilichopo Mkoani Mbeya, pamoja na Kituo cha Nkangamo kilichopo Tunduma, mkoani Songwe, ambapo  amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO iko imara katika kutekeleza miradi na  kuwahudumia wananchi.

Hii ni ziara maalumu aliyoifanya katika mikoa ya kusini ambapo licha ya kukutana na wafanyakazi wa mikoa hiyo, ametembelea vituo vya kuzalisha umeme kwa gesi asilia Mtwara 1 na 2, pamoja na Miradi mbalimbali ikiwemo Kituo cha kupoza umeme Songea – Tunduru, Kituo cha kupoza umeme Mradi wa TAZA Malangali – Sumbawanga, Kituo cha kupoza umeme Nkangamo Tunduma – Songwe, Kituo cha kupoza umeme Iganjo Mbeya pamoja na njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kilovoti 400(km 203) Tunduma – Sumbawanga.

 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO