MANISPAA KIBAHA YAADHIMISHA SIKU YA USAFI WA MAZINGIRA DUNIANI KWA KUFANYA USAFI KATIKA MAENEO MBALIMBALI



Kibaha, Pwani – Septemba 20, 2025

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeadhimisha kilele cha Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ikiwemo jengo la utawala la Ofisi ya Mkurugenzi, vituo vya abiria, maeneo ya wazi, pamoja na barabara za watembea kwa miguu.

Maadhimisho hayo yameongozwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Catherine Saguti, ambaye amewaongoza wananchi na watumishi wa Halmashauri kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Tunza Mazingira kwa Kuzipa Taka Thamani", ikihamasisha jamii kuona taka kama rasilimali inayoweza kurejelewa au kutumika kwa namna nyingine badala ya kuwa uchafu unaodhuru mazingira.

Akizungumza na wananchi, Dkt. Saguti aliwapongeza kwa kujitokeza kushiriki zoezi hilo, na kutoa wito kwa watendaji wa kata na mitaa kuendeleza kampeni za usafi ili kuzuia magonjwa ya milipuko.


“Mazingira safi yanamaanisha afya bora. Tukihamasisha usafi kwenye kila mtaa, tutaokoa maisha na kupunguza mzigo wa magonjwa katika jamii yetu,” alisema Dkt. Saguti.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Manispaa hiyo, Bw. Issa Hassan, alisema Halmashauri inaendelea kubuni mbinu za kuhamasisha usafi, ikiwemo kushindanisha mitaa ili kutambua na kutoa motisha kwa wale wanaofanya vizuri.

Katika mashindano hayo ya usafi, mitaa iliyoibuka kidedea ni kama ifuatavyo:

Mtaa wa Mkoni A

Mtaa wa Kwa Mfipa – Kata ya Kibaha

Mtaa wa Uyaoni – Kata ya Maili Moja

Bw. Hassan amesema kuwa lengo la ushindani huo ni kuongeza ari ya usafi kwa jamii nzima na kuifanya Manispaa ya Kibaha kuwa mfano bora wa utekelezaji wa ajenda ya mazingira safi na salama.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO