*SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIKI (IAEA) KUISAIDIA TANZANIA UZALISHAJI UMEME WA NYUKLIA*



๐Ÿ“Œ *IAEA na Tanzania kushirikiana  kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa uzalishaji umeme wa nyuklia*

๐Ÿ“Œ *Mhandisi Mramba aishukuru IAEA kuunga mkono dhamira ya Tanzania kuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati*

Vienna, Austria. 

Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomi (IAEA) limeeleza nia yake ya kuisaidia Tanzania katika mipango yake ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Nyuklia 

Hayo yamebainika katika kikao kando ya Mkutano Mkuu wa 69 wa masuala ya Atomic uliohitimishwa tarehe 19 Septemba, 2025 nchini Austria.

Kikao hicho kilifanyika kati ya Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Prof. Carolyne Nombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Nyuklia wa IAEA Bi Liliya Dullinet.

Kikao hicho kimekuwa sehemu ya mwendelezo wa mazungumzo ya ushirikiano kati ya Tanzania na IAEA, kikilenga kuharakisha utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kuzalisha umeme kwa kutumia nyuklia. 

Katika mazungumzo hayo, IAEA imeahidi kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika maeneo kadhaa ya kipaumbele yakiwemo Msaada wa Kiufundi na Kitaalamu kwa kusaidia Tanzania katika nyanja zote za maandalizi ya miundombinu ya nyuklia.

 Eneo lingine ni Mafunzo kwa Wataalamu wa ndani katika kujenga uwezo wa kitaalamu kwa watanzania ili kushiriki moja kwa moja katika maandalizi na uendeshaji wa miradi ya nyuklia ambapo tayari IAEA imetoa nafasi za masomo kwa Tanzania. 

Shirika hilo pia limeonesha utayari wa kuisaidia Tanzania katika kufanya Maboresho ya Mfumo wa Kisheria na Kisera kwa kutoa mwongozo katika kuimarisha sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa miradi ya nyuklia.

Aidha, katika hatua nyingine IAEA na Tanzania zimekubalians kuandaa kwa pamoja Mpango Kazi wa Taifa wa Utekelezaji wa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia kuanzia hatua ya Maandalizi. 

Vilevile, Shirika hilo limeonesha utayari wa kuandaa ziara za mafunzo kwa Viongozi na wataalam wa Tanzania ili kupata uelewa na Kubadilishana uzoefu katika masuala ya teknolojia ya Nyuklia katika kuzalisha umeme. 

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba aliwashukuru IAEA kwa utayari wao wa kuisaidia Tanzania. Pia alisisitiza kuwa dhamira ya Tanzania kuanza safari ya kuzalisha umeme wa nyuklia ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati.

Wajumbe wengine walioshiriki kikao hicho ni Mha. Joseph Kirangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Maji na Madini kutoka Zanzibar, Mha. Athuman Kilundumya Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Prof. Najat Mohamed,  Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Nguvu za Atomi Tanzania (TAEC), Mha Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu na Wataalam wa masuala ya Nyuklia.


Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO