KUNAMBI AWATAKA WAKAZI WA KILIMANJARO KUMPA KURA ZA KISHINDO DKT. SAMIA SULUHU HASSAN
KUNAMBI AWATAKA WAKAZI WA KILIMANJARO KUMPA KURA ZA KISHINDO DKT. SAMIA SULUHU HASSAN.
Na Mwandishi Wetu,
Moshi, Kilimanjaro.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Suzan Kunambi, amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kumpa kura za kishindo mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, akisema ni kiongozi jasiri, muadilifu na mwenye dhamira ya kweli ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Kunambi alitoa wito huo Oktoba 8, 2025, wakati akizungumza katika mkutano wa wanawake uliofanyika katika Kata ya Uru Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
Amesema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake, amefanikisha maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, barabara, maji na miradi mingine ya kijamii.
“Tunakuja kwenu kwa unyenyekevu mkubwa kuwaombea kura wagombea wetu wote kuanzia kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa CCM. Mnaijua mipango ya chama, na jukumu lenu ni kufuatilia utekelezaji wa ahadi tulizotoa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2025–2030,” alisema Kunambi.
![]() |
| Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Suzan Kunambi, akizungumza na wanawake wa Wilaya ya Moshi vijijini. |
Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini ni matokeo ya uongozi thabiti na wenye dira wa viongozi wa CCM. Alionya dhidi ya watu wanaojaribu kuibua chokochoko wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, mgombea wa ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Maleko, amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia imeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuiamini CCM kama chama kinachojali ustawi wa wananchi wake.
Akizungumza, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kilimanjaro, Elizabeth Minde, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kumuombea kura Rais Samia, akisema wanawake ni nguzo muhimu katika kuhakikisha ushindi wa chama hicho.
![]() |
| Mgombea wa ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Maleko, akizungumza na wanawake wa Wilaya ya Moshi vijijini. |
“Wanawake ni watu wa mipango na umoja. Tukiungana, hakuna lisilowezekana,” alisema Minde.
Mwisho.
#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update
Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX
karibu sana.



Comments
Post a Comment