RC KILIMANJARO ATOA ONYO KALI DHIDI YA MAANDAMANO WAKATI WA UCHAGUZI.

RC KILIMANJARO ATOA ONYO KALI DHIDI YA MAANDAMANO WAKATI WA UCHAGUZI.

Na Musa Mathias,
Same, Kilimanjaro.

Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa. https://youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=I4xrm3DGzDSHWbuH

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, amewaonya vikali baadhi ya wananchi wanaopanga kufanya vurugu na maandamano mkoani humo katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Babu ametoa onyo hilo wakati akizungumza kwenye kongamano la wanawake wilayani Same lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nzoroko, likihudhuriwa na zaidi ya wanawake 300.

Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umejipanga kuhakikisha usalama unakuwepo kabla, wakati na baada ya uchaguzi, huku akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani.
“Serikali ya mkoa na wilaya tumejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo. Nendeni mkapige kura kwa amani. Mkoa wa Kilimanjaro si wa vurugu, wala watu wake hawataki maandamano. Wale wanaotaka kufanya maandamano watafute nchi nyingine ya kufanya maandamano,” amesema Nurdin Babu.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi kwa amani na utulivu bila vitisho wala usumbufu. Amesisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuvuruga utaratibu wa uchaguzi atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali nafasi aliyonayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuhamasisha wanawake kujitokeza kupiga kura na pia kujengeana uwezo katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uongozi, ujasiriamali, afya ya akili, nidhamu ya fedha, na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Kasilda amesema elimu ya afya ya akili ni muhimu kwa wanawake ili waweze kuendesha familia kwa utulivu na kuepuka msongo wa mawazo unaochochewa na changamoto za maisha ya kila siku. Aidha, amewataka wanawake kutumia nishati safi ya kupikia kama gesi na majiko banifu ili kulinda afya zao na mazingira.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya kifedha, akiwataka wanawake kutumia mikopo na mitaji wanayopewa kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuimarisha kipato na kukuza uchumi wa familia.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Same, Bi. Saumu Mndeme, amesema makongamano hayo hufanyika kila mwaka na yameleta matokeo chanya katika nyanja za uongozi, ujasiriamali, elimu ya fedha na uwezeshaji wa wanawake.
Ameongeza kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wanawake, viongozi wa serikali, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo kujadili changamoto zinazowakabili wanawake na kutoa suluhisho endelevu.

Katika hatua nyingine, washiriki wa kongamano hilo wamepata elimu juu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ambapo wanawake wametakiwa kuripoti matukio yote ya ukatili kwa vyombo husika na kuepuka kulinda wahalifu kwa visingizio vya kifamilia.

Kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo “WANAWAKE NA UONGOZI: Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025,” na limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wawakilishi wa taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo, pamoja na wanawake zaidi ya 300 kutoka kata zote za Wilaya ya Same.

Washiriki walipata nafasi ya kujadili kwa kina namna ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kitaifa, kulinda afya ya familia, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia miradi ya kikundi na teknolojia bunifu za kidigitali.






Mwisho.

#KipeoOnlineMedia #Habari #Tanzania #News #Update Asante kwa kusoma Kipeo Online Media. Tembelea kipeoonlinemedia.blogspot.com kwa habari zaidi, Subscribe Channel yetu ya Youtube hapa youtube.com/@kipeoonlinemedia?si=vZ45foO1hBmK1xvX karibu sana.

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO