NMB YAKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO KWA AJILI YA “NMB MBUZI CUP 2025” KATIKA SHULE YA SEKONDARI SAME
Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Katika kuendeleza juhudi za kuunga mkono maendeleo ya vijana na kukuza vipaji kupitia michezo, Benki ya NMB imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa Shule ya Sekondari Same kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya mabweni maarufu kama “NMB Mbuzi Cup 2025.”
Mashindano haya yalianza rasmi jana, Jumamosi tarehe 20 Septemba 2025, yakihusisha ushindani mkali baina ya mabweni yote ya shule hiyo katika michezo mitatu: mpira wa miguu (football), mpira wa mikono (handball), na mpira wa wavu (volleyball). Hii ni sehemu ya muendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya NMB na shule hiyo, ambapo wanafunzi wote wa Same Sekondari – asilimia 100 – tayari wamefungua akaunti za vijana kwa ajili ya matumizi yao wakiwa shuleni na hata baada ya kuhitimu.
Katika kuashiria uzinduzi wa mashindano hayo, mechi ya ngao ya hisani ilichezwa kati ya wanafunzi wa kidato cha sita dhidi ya kidato cha tano, ambapo kidato cha sita waliibuka washindi kwa mabao 3–2. Mechi hiyo ya ufunguzi iliibua hisia, ikionesha kiwango kizuri cha ushindani, na kutoa ladha ya burudani kubwa inayosubiriwa katika mashindano yajayo.
Mashindano ya NMB Mbuzi Cup 2025 yanatarajiwa kudumu kwa takribani siku kumi, yakitoa jukwaa la kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo miongoni mwa wanafunzi, huku yakisisitiza mshikamano, nidhamu, na matumizi bora ya muda wa mapumziko ya masomo.
Mshindi wa kila mchezo atazawadiwa mbuzi mzima kama ishara ya ushindi na motisha kwa wachezaji, sambamba na zawadi nyingine za heshima kwa timu bora na wachezaji mahiri, zitakazotolewa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na uongozi wa shule. Zawadi hizi zinatarajiwa kuongeza ari kwa washiriki na kuhimiza ushindani wa kweli na wa heshima katika kila mchezo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano hayo anatarajiwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Mamndolwa Gembe, ambaye atazindua rasmi tukio hilo kesho, tarehe 22 Septemba 2025, mbele ya viongozi wa shule, walimu, wanafunzi, na wawakilishi kutoka Benki ya NMB.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa vya michezo, Bwana Saad Masawila, Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Same, alisema:
“Benki ya NMB imeendelea kuwa mshirika mkuu wa maendeleo ya elimu na michezo nchini. Tunaamini kwamba michezo si tu burudani bali ni nyenzo muhimu ya kukuza nidhamu, mshikamano, na uongozi kwa vijana wetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya ndoto za wanafunzi wa Same Sekondari.”
Kwa mujibu wa uongozi wa shule pamoja na Benki ya NMB, mashindano haya yanalenga si tu kukuza vipaji vya michezo, bali pia kuchangia katika malezi bora ya vijana, kuwaelimisha juu ya usimamizi wa rasilimali kupitia akaunti za benki, pamoja na kuimarisha umoja wa kijamii miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo.
Comments
Post a Comment