UJENZI MRADI WA TAZA WAFIKIA ASILIMIA 58 KWA UPANDE WA TANZANIA



*📌Nguzo 420 za kusafirisha umeme wa kV 400 zasimikwa*

*📌Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania kwa kasi ya utekelezaji wa mradi*

*📌Wakandarasi waishukuru Serikali kutoa fedha kwa wakati*

Ujenzi wa mradi wa usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 400 unaounganisha Tanzania na Zambia( TAZA) umefikia asilimia 58 ya uekelezaji wake kwa upande wa Tanzania.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu,  Mhandisi Sadick Mwaifunga  wakati wa ziara ya ukaguzi na tathmini ya utekelezaji wa mradi huo inayohusisha watendaji wa Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) pamoja na Benki ya Dunia(WB).

Ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa mradi katika  mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa kwa kukagua ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Kisada- Iringa, Iganjo-Mbeya hadi kituo cha kupoza umeme cha Malangali Sumbawanga yenye urefu wa Kilometa 616 pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme  Katika mikoa hiyo.

"Mpaka sasa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 58 ikihusisha  ujenzi wa miundombinu ya njia kusafirisha umeme pamoja  vituo vya kupoza umeme" Amesema Mhandisi Mwaifunga


Amefafanua kuwa,  ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa - Kisada; Kisada - Mbeya; Mbeya - Tunduma na Tunduma - Sumbawanga umefikia asilimia 81.

Pia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme Iringa, Kisada, Mbeya, Tunduma na Sumbawanga umefikia asilimia 35.

Mha. Mwaifunga amesema katika Mradi huo jumla ya nguzo 1614 za umeme wa kV 400 zitajengwa kwa urefu wa Kilometa 616.

Aidha, ameeleza kuwa hadi sasa tayari zaidi ya nguzo 420 zimeshasimikwa na   zoezi hilo linaendelea.


Kwa Upande wake Msimamizi wa Mradi huo kutoka Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), Mhandisi Elias Makunga amewataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili kukabiliana na changamoto ya hali ya hewa hasa nchi inapoelekea katika kipindi mvua.

Amesema wakandarasi wanamuda mwingi wa kufanya kazi kipindi cha kiangazi hivyo watumie kipindi hicho kufidia Kazi zitakazosimama wakati wa kipindi cha mvua.

" Hatutamani kuona mkandarasi anasingizia mvua  kuwa imekwamisha utendaji wake  wa kazi, ni vyema sasa  kipindi hiki cha kiangazi kazi zifanyike kwa kasi kubwa ili kutochelewesha mradi huu unaosubiriwa kwa hamu kubwa" amesisitiza Mha. Makunga


Benki ya Dunia kwa upande wake  imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia vyema mradi huo hasa kwa hatua nzuri  ya utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake Meneja Mradi kwa upande wa  Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Kisada Iringa hadi Mbeya, Mhandisi Ananthan Pannerselvam ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa wakati za  utekeleza miradi huo.

Amesema  kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na mpaka sasa hakuna changamoto yoyote inayoweza  kuhatarisha utekelezaji ambapo ameahidi kukamilisha kazi kwa wakati.



Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO