SERIKALI YAONDOA VAT KWA VITUO VYA GESI ASILIA ILIYOSHINDILIWA (CNG)*
📌 *Lengo ni kuongeza uwanda wa matumizi ya CNG katika vyombo vya moto nchini*
📌 *Mhandisi Mramba azindua kituo cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa ( CNG) cha PUMA Energy*
📌 *Asema vifaa vya kuwekea mifumo ya gesi kwenye vyombo vya moto pia imeondolewa*
📌 *Apongeza PUMA Energy kwa kuiunga mkono Serikali katika ujenzi wa vituo vya CNG*
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba amesema Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vituo vyote vya Gesi iliyoshindiliwa (CNG) nchini ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya moto kupitia uwepo wa vituo vingi vya kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Amesema kuwa Serikali pia imeondoa kodi kwenye vifaa vya kuwekea mifumo hiyo ya gesi kwenye vyombo vya moto kama vile magari na bajaji ikiwa ni hatua pia ya kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika vyombo vya moto.
Mhandisi Mramba ameeleza hayo leo Septemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) cha kampuni ya Puma Energy kilichopo Bagamoyo road.
" Serikali inafanya jitihada hizi ili kutoa nafasi kwa watanzania kutumia gesi kwenye vyombo vyao vya moto kwa kurahisisha mazingira ya upatikanaji wake na pia kwa kuwa kuna unafuu wa gharama pale unapotumia Gesi Asilia ikilinganishwa na mafuta". Amesema Mramba
Mramba amesema kwa sasa kuna vituo 11 vya kujaza gesi kwenye magari jijini Dar es Salaam ambapo Serikali imedhamiria kuwa hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu idadi ya vituo hivyo itakuwa imeongezeka na kufika 18 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, ameeleza kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeshaleta magari sita yatakayokuwa yanazunguka kujaza gesi kwenye magari katika maeneo mbalimbali.
Katika hatua nyingine Mha. Mramba ameipongeza PUMA kwa ujenzi wa kituo hicho na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwekeza katika vituo hivyo vya CNG.
“Natoa wito pia kwa Wananchi na watumiaji wa vyombo vya moto kuweza kutumia gesi asilia kwani vituo vimeongezeka nchini na hivyo kupelekea huduma kuwa karibu na jamii zetu". Amesisitiza Mha. Mramba
Kwa upande wake, Bi. Fatma Abdallah ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy amesema kampuni hiyo imejenga kituo hicho ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika mageuzi ya matumizi ya nishati ambayo ni safi na salama katika kuendesha vyombo vya moto.
Comments
Post a Comment