TANZANIA YANG’ARA UWEKEZAJI KATIKA ELIMU KWA RASLIMALI ZA NDANI*
📌 *Dkt. Biteko asema tafiti zaonesha elimu bora huchangia asilimia 20-30 ya ukuaji wa uchumi*
📌 *Walimu milioni 17 wa shule za msingi na sekondari wahitajika Afrika ifikapo 2030*
📌 *Bajeti ya elimu yaongezeka kwa trilioni 1.44 tangu mwaka 2020/21*
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika matumizi ya rasilimali za ndani na kuwekeza katika sekta ya elimu kwa maendeleo endelevu.
Amesema hayo leo Septemba 24, 2025 jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Tano la Kimataifa la Elimu Bora lililoongozwa na kauli mbiu inayosema “Kuimarisha mifumo na uwekezaji: Kusonga mbele katika Uhamasishaji wa Rasilimali za Ndani kwa ajili ya Elimu Jumuishi, Bora na Endelevu Barani Afrika”.
Dkt. Biteko ametaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kutunga na kuboresha Sera, Sheria na miongozo mbalimbali ya elimu, kuongeza kiwango cha bajeti ya elimu kutoka shilingi za trilioni 4.72 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia shilingi za trilioni 6.16 mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema ongezeko hilo la bajeti limeboresha mazingira na miundombinu mbalimbali ya elimu kwa maendeleo endelevu. Vile vile, Serikali imetanua wigo wa Sera ya Elimu bila malipo kwa elimu ya Sekondari ambapo mwaka 2020 kilitengwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 312.08 na mwaka 2024 kilitengwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 796.58 ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 484.
“Ongezeko hili limeweza kupunguza changamoto za kifedha zinazorudisha nyuma sekta ya elimu na hivyo kuongeza idadi ya wanufaika wa elimu malipo kutoka wanafunzi 14,940,925 wa mwaka 2020 hadi kufikia wanufaika 16,155,282 wa mwaka 2024,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Pamoja na mafanikio haya, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto nyingine kadhaa katika sekta ya elimu kwa maendeleo endelevu.”
Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuifanyia kazi kauli mbiu ya mwaka huu ili kufikia utekelezaji wa matakwa ya kimataifa ya kutenga na kuelekeza asilimia 20 ya bajeti ya nchi katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Aidha, amesema Afrika ikiwekeza katika elimu bora itaweza kutatua changamoto ya uhaba wa walimu bora hususan maeneo ya vijijini. Ambapo, hadi kufikia mwaka 2030 Bara hilo linahitaji kuwa na walimu milioni 17 ili kuwa na elimu bora ya msingi na sekondari na kuwa na mifumo thabiti ya elimu ya kidigitali ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo nakuendana na mazingira tuliyonayo.
Ambapo tafiti za Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) mwaka 2025 zinaonesha kwamba, elimu bora, kwa wastani, huchangia asilimia 20 hadi asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi wa muda mrefu wa Taifa lolote. Tafiti hizo hizo pia zinaonesha kuwa, mtu mwenye elimu ya juu hupata kipato kwa wastani wa asilimia 50 hadi asilimia 100 zaidi ya mtu asiyekuwa na elimu hiyo ya juu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo amesema suala la kugema raslimali fedha na watu vinaweza kuongeza ubora wa elimu na kupunguza changamoto za sekta ya hiyo kwa kushirikiana na wadau.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Kongamano hilo linalenga kuboresha sekta ya elimu nchini na kuwa Wizara yake ina jukumu la kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa katika viwango vya kimataifa.
“ Kongamano hili limekuja katika wakati muafaka ambapo Serikali inaendelea kuwekeza raslimali fedha, hivyo mkutano huo utasaidia kugema raslimali fedha ili kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu,” amesema Prof. Nombo.
Meneja wa Kanda wa Global Partnership for Education (GPE), Belay Addise amesema kuwa Taasisi hiyo inajivunia ushirikiano wake mzuri uliopo kati yake na Serikali ya Tanzania tangu mwaka 2013. Ambapo kupitia ushirikiano huo Tanzania imepokea takribani dola za Marekani milioni 348 kupitia mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF, UNESCO na Swedish Development Agency (SIDA) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya elimu.
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Martha Makala ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wa elimu kutoka ndani na nje nchi kwa kuwezesha Kongamani hilo na kuwa uwepo wa watunga sera katika Kongamano hilo utasaidia kufanya mijadala kuwa yenye tija itakayoleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.
Comments
Post a Comment