DODOMA YAPOKEA UJUMBE KUTOKA MALAWI: UMEFIKA KUJIFUNZA USIMAMIZI RASILIMALI MADINI*
*Kaimu RC Kazungu: Tanzania imepiga hatua kubwa usimamizi wa rasilimali madini*
*Wizara, Tume ya Madini zatoa elimu ya madini kwa ujumbe kutoka Malawi*
📍 Dodoma,
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Khatibu Kazungu amepokea ujumbe maalum kutoka nchini Malawi uliowasili nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa rasilimali madini.
Ujumbe huo, umeongozwa na Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Biashara ya Vikundi Zizwan Khonje akiwa ameongozana na wadau wa Sekta ya Madini akiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi na maafisa mbalimbali wa mabenki wa nchini humo na kupokelewa rasmi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma, ambapo umeeleza dhamira yake ya kujifunza kutoka Tanzania kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika kusimamia sekta ya madini kwa uwazi, tija na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa kuupokea ujumbe huo, Dkt. Kazungu amewapongeza wageni hao kwa kuichagua Tanzania kama kituo cha maarifa na uzoefu katika sekta ya madini huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kutambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuleta mageuzi katika sekta hiyo muhimu.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Serikali ya Tanzania, nawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Uamuzi wenu wa kuja kujifunza kwetu ni ushahidi wa wazi kuwa tunapiga hatua kubwa katika usimamizi bora wa rasilimali zetu, hasa madini. Hili ni jambo la kujivunia kama taifa,” amesema Dkt. Kazungu.
Dkt. Kazungu ameeleza kuwa Tanzania, kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake imefanikiwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa shughuli za utafutaji, uchimbaji, biashara, na usafirishaji wa madini, huku ikizingatia kanuni za uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yanayozungukwa na shughuli za madini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Biashara ya Vikundi Zizwan Khonje kutoka Malawi ameonesha kufurahishwa na mapokezi mazuri waliyopewa, na kusisitiza kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika Afrika kwa kuwa na sera na mifumo ya usimamizi wa madini inayojali maslahi ya taifa na wananchi.
Khonje amesema, lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna ambavyo Wizara ya Madini ya Tanzania imefanikiwa katika usimamizi na urasimishaji wa wachimbaji wadogo, uendeshaji wa masoko ya madini na viwanda vya uongezaji thamani madini.
Ameongeza kuwa, wakiwa nchini ujumbe huo unatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali yanayohusiana na uchimbaji, uchenjuaji usafishaji na biashara ya madini ambapo kwa jiji la Dodoma ujumbe huo ametembelea kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Eyes of Africa kwa lengo la kujifunza kwa vitendo mbinu na mifumo inayotumika.
Awali, ujumbe huo ulitembelea Ofisi za Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma ambapo walipata fursa ya kupitishwa kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inayotumika katika usimamizi wa Sekta ya Madini pia, walipitishwa kuhusu uongezaji thamani madini, usimamizi wa leseni, biashara na masoko ya madini.
Tanzania na Malawi zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali, na ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda hususan katika utawala bora wa rasilimali za asili, ambazo ni mhimili wa maendeleo endelevu ya mataifa ya Afrika.
Comments
Post a Comment