RAS NZOWA: KAMILISHENI MIRADI KWA WAKATI
RAS NZOWA: KAMILISHENI MIRADI KWA WAKATI
Na Musa Mathias.
Same - Kilimanjaro.
Same - Kilimanjaro.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Nzowa, ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha inakamilisha kwa wakati miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ya Awamu ya Sita, ili wananchi waanze kunufaika mapema na huduma bora.
Bw. Nzowa ametoa maagizo hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Same, alipoambatana na Sekretarieti ya Mkoa na kukagua miradi mitatu ya maendeleo sekta ya elimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1. Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuona kila mradi unakamilika kwa muda uliopangwa, kwa viwango bora, na kuanza kutoa huduma kwa wananchi bila ucheleweshaji.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Amali, Kata ya Kihurio, unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 584 na unatarajiwa kuanza kutumika Januari 2026 kwa kudahiri wanafunzi 80 katika mikondo miwili.
Mradi mwingine ni ujenzi wa bwalo la chakula la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Ndungu unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 205, na ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Misufini Goma kwa zaidi ya shilingi milioni 389, unaojumuisha madarasa manne, mabweni mawili (wavulana na wasichana) pamoja na matumdu 14 ya vyoo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Alibainisha kuwa serikali itaendelea kusimamia miradi kwa ukaribu ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango bora, akisisitiza kuwa miradi yenye ubora wa juu ndiyo inayodumu kwa muda mrefu na kuwa chachu ya maendeleo endelevu.
Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hii inatarajiwa kukamilika kabla ya octoba 30, mwaka huu, inathibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi, wanapata huduma za kijamii kwa urahisi na ubora, sambamba na kukuza elimu na maendeleo ya watu.
Mwisho.
Comments
Post a Comment