KASIKI AWAPIGA MSASA WADAU WA SEKTA YA MADINI*


- *Abainisha fursa kubwa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani*

*Ajira zaongezeka mara tatu tangu 2018*

MKURUGENZI wa Ukaguzi na Biashara ya Madini katika Tume ya Madini (MATD), CPA. Venance Kasiki, amewataka wadau wa Sekta ya Madini kuongeza ubunifu na ushiriki endelevu kwenye shughuli za uchumi wa madini kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazohitajika migodini badala ya kuendelea kuwa mawakala wa wazalishaji wa kigeni (OEMs).

Akizungumza  katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita, Kasiki alisema ushiriki wenye tija unahitaji kampuni kuwa na mifumo madhubuti ya uendeshaji na usimamizi, kutoa bidhaa na huduma bora kwa wakati, kujifunza teknolojia mpya, pamoja na kushirikiana katika kuunda mitaji mikubwa ya pamoja.

Alibainisha kuwa mnyororo wa thamani wa madini una fursa nyingi zinazoweza kushughulikiwa na Watanzania ikiwemo usambazaji wa mitambo ya migodini, huduma za TEHAMA, usafirishaji, fedha na bima, huduma za vyakula, vifaa kinga (PPE), famasia na vifaa tiba, ulinzi, uchorongaji, usafi na nyingine nyingi.


“Ni wakati sasa kwa wadau wa sekta hii kutumia ipasavyo fursa zilizopo huku wakizingatia sheria na kanuni zilizowekwa, ili kuongeza tija kwa taifa,” alisisitiza Kasiki.

Akizungumzia mchango wa sekta hiyo katika ajira, Kasiki alisema mwaka 2018 kulikuwa na ajira 6,668 kwa Watanzania na 335 kwa wageni. Hata hivyo, ifikapo mwaka 2024 idadi hiyo imeongezeka maradufu na kufikia zaidi ya Watanzania 19,371 na wageni 503.

“Hii ni ishara tosha kuwa mchango wa Sekta ya Madini katika kutoa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa unaongezeka kwa kasi,” alisema.


Hata hivyo, alitaja baadhi ya changamoto zinazoibuka kwenye zabuni na manunuzi kuwa ni pamoja na kutofuata taratibu za EOI na RFP, kuwepo kwa vigezo visivyo shindanishi vinavyolenga kampuni maalum, ushindani usio na tija kwa wazalishaji wa ndani, ubia usiokidhi matakwa ya kisheria na utoaji wa bidhaa au huduma zisizokidhi viwango.

“Tume ya Madini itaendelea kusimamia Sheria ya Madini na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania ili kuhakikisha sekta hii inawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla,” aliongeza.

Aidha, Kasiki aliwaasa Watanzania kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazotumika migodini katika eneo la Buzwagi mkoani Geita, ambapo Serikali imetenga eneo maalum kwa ajili ya uwekezaji huo.


 

Comments

Popular posts from this blog

HATMA YA TAIFA IPO KATIKA USAWA WA KIJINSIA, SIO VIWANDA PEKEE.

MSAKO MKALI KUREJESHA HALI ya USALAMA TANGA, WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA

PJT-MMMAM YAWEZESHA UANZISHWAJI WA VITUO 206 VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO