MWANZA PRECIOUS METALS REFINERY YAKUSANYA ZAIDI YA TANI 5 ZA DHAHABU KWA NIABA YA BOT
📍Mwanza
Kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) kilichopo jijini Mwanza, kimefanikiwa kukusanya zaidi ya tani tano za dhahabu kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Hayo yamesemwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Nyaisara Mgaya, alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka nchini Malawi uliotembelea mkoani humo kwa lengo la kujifunza kuhusu usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini, hususan mfumo wa masoko unaotumika nchini Tanzania.
Mhandisi Mgaya amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha hadi kilo 960 za dhahabu kwa siku, ingawa kwa sasa kinatumia mashine zenye uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku, kutokana na upatikanaji wa malighafi.
Katika kikao hicho, kiongozi wa ujumbe kutoka Malawi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi nchini humo, Zizwan Khonje, amemshukuru Afisa Madini wa Mkoa wa Mwanza kwa elimu waliyoipata kuhusu mfumo wa biashara na masoko ya madini hapa nchini.
“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua katika kuboresha Sekta ya Madini, ikiwemo uanzishwaji wa masoko ya madini ya wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa rasilimali hizi,” amesema Khonje.
Awali, ujumbe huo ulipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambako walipokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Balandya Elikana, ambaye aliwakaribisha rasmi mkoani humo.
Ziara hiyo ya ujumbe kutoka Malawi inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini ya nchi hiyo kwa kuimarisha mifumo ya uwazi, kuongeza mapato ya serikali, na kuwezesha ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo kwenye soko la kimataifa la madini.
Comments
Post a Comment